WAKATI jana wakihitimisha kwa mafanikio tamasha la kila mwaka la 'Simba Day' lililofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, klabu ya Simba inajiandaa kumpiga bei winga wake, Onana, imefahamika.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema klabu ya Muaither ya nchini Qatar imetuma ofa ya Dola za kimarekani 100,000 kama ada ya uhamisho na pesa kama hizo pia ikiwa ni ya mchezaji mwenyewe kwa ajili ya kusaini mkataba mpya na klabu hiyo.
Taarifa zinasema Onana hakuwa mmoja wa wachezaji waliofanya mazoezi na kikosi hicho kuelekea katika mechi ya tamasha la Simba Day jana.
"Ni kweli ipo hiyo ofa, na wala viongozi hawana tatizo na hilo kwa sababu kama utakumbuka alichelewa kujiunga na kambi kwa kuwa kulikuwa na mpango wa kuvunja naye mkataba lakini kufeli kwa dili ya Elie Mpanzu kukamwokoa. Ila sasa usajili wa Moussa Kamara nao umechangia kuuzwa kwa sababu inaonekana hakuna uwezekano wa kumkata Ayoub Lakred ambaye ameumia na atakaa nje kwa muda wa wiki sita," alisema mtoa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo.
Alisema awali Simba ilitaka kuliondoa jina la Ayoub Lakred kwenye orodha ya wachezaji 12 wa kigeni ili liingizwe la Kamara lakini dili la Onana limesababisha mpango huo kusitishwa.
"Kwa maana hiyo Simba itakuwa na makipa wawili wa kigeni msimu ujao, na imelazimika kufanya hivyo kwa sababu Ayoub atakaa nje wiki sita sawa na mwezi mzima, lakini ameongezeka uzito, hivyo akipona ana kazi nyingine ya kupunguza uzito, hiyo ni miezi miwili wakati timu inakabiliwa na michezo muhimu mwanzoni tu mwa msimu," alisema mtoa taarifa.
Kabla ya klabu hiyo kuleta ofa, Onana anayecheza nafasi ya winga wa kushoto, alikuwa anatakiwa na klabu za Kaizer Chiefs, Orlando Pirates za Afrika Kusini na Wydad Casablanca ya Morocco.
Mchezaji huyo raia wa Cameroon, alisajiliwa na klabu hiyo mwanzoni mwa msimu uliopita akitokea klabu ya Rayon Sport ya Rwanda.
Onana akiondoka Simba ataungana na nyota wengine, Clatous Chama, Henock Inonga, Sadio Kanoute na Saido Ntibazonkiza kuachana na timu hiyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED