Simba yatamba kuendeleza dozi

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 09:30 AM Aug 25 2024
Kocha Mkuu, Fadlu Davids,.
Picha:Simba
Kocha Mkuu, Fadlu Davids,.

KIKOSI cha Simba leo kitashuka tena Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam kucheza mchezo wa pili wa Ligi Kuu, Tanzania Bara dhidi ya Fountain Gate, huku Kocha Mkuu, Fadlu Davids, akisema wanataka kuendeleza wimbi la ushindi kama walivyofanya Jumapili iliyopita katika uwanja huo dhidi ya Tabora United.

Simba inakwenda kucheza mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mabao 3-0 katika mchezo wao kwanza wa Ligi hiyo.

Fadlu amesema hawatarajii tena kufanya makosa ya kusubiri kuwa na uhakika wa ushindi kipindi cha pili, badala yake wanataka kuimaliza mechi mapema.

"Nakumbuka mechi iliyopita hatukuimaliza kipindi cha kwanza, tukalazimika tufanye hivyo kipindi cha pili, hatutarajii tena kufanya hivyo, ila kizuri tulichokifanya katika mechi iliyopita dhidi ya Tabora United ni kulinda, hatukuruhusu wapinzani wapige shuti hata moja lililolenga lango, hili tutataka kuendelea nalo," alisema kocha huyo raia wa Afrika Kusini.

Pamoja na hayo, kocha huyo amekiri kuwa mchezo hautokuwa rahisi kwani kwa muda mfupi tu alivyowafuatilia wapinzani wake amegundua kuwa wana uwezo mkubwa wa kujilinda.

"Nafikiri Fountain Gate ni timu nzuri hasa sehemu ya ulinzi kwa jinsi nilivyoisoma kwa siku chache, kwa hiyo tumejiandaa vyema, tunakwenda kwenye mchezo huo tukiwa makini na kuheshimu wapinzani wetu.

Ni mechi ambayo naona wapinzani wetu watakaa nyuma, na sisi tutafanya kazi ya kuifungua, inatakiwa tunapopata nafasi tuitumie ili kurahisisha mchezo kwani tukipata mabao watafunguka, mchezo utaanza kuwa wa wazi," alisema Fadlu.

Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Mohamed Muya, amesema wanaiheshimu Simba lakini hawaiogopi, hivyo wasitarajie kupata ushindi kirahisi.

"Tunaiheshimu Simba, ni timu kubwa na yenye uwekezaji mkubwa, lakini sisi ni wazuri na tumewekeza vizuri, wachezaji wamepata mafunzo mazuri na ni wachapakazi kweli kweli, nao wana kiu ya kupata maendeleo kwenye mchezo wa soka.

Kwa maandalizi tuliyowapa wachezaji wetu na morali waliyonayo, tuna imani tutaonyesha mpira mzuri na mashabiki watapata burudani safi," alisema kocha huyo.

Wakati Simba ikingia katika mchezo huo ikiwa na pointi tatu, ikicheza mechi moja, kwa upande wa Fountaine Gate utakuwa mchezo wao wa kwanza kwenye Ligi Kuu msimu huu.

Katika hatuanyingine, Klabu ya Simba sasa rasmi watavaana na Al Ahly Tripoli ya Libya katika mchezo wa raundi ya kwanza, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Hii ni baada ya juzi timu hiyo kuitandika Uhamiaji ya Zanzibar mabao 3-1 katika mchezo wa marudiano hatua ya awali uliochezwa Juni 11, Tripoli nchini Libya.

Timu hiyo imetinga raundi ya kwanza kwa jumla ya mabao 5-1, kwani katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Jumapili iliyopita, ilishinda mabao 2-0.

Kwa matokeo hayo, Simba itaanzia ugenini, Septemba 13 nchini Libya, kabla ya mchezo wa marudiano kuchezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Septemba 20.