Simba yasaka mshambuliaji

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 10:26 AM Aug 11 2024
Kocha Mkuu, Fadlu David.
Picha: Simba SC
Kocha Mkuu, Fadlu David.

BAADA ya mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na kuchapwa bao 1-0, viongozi wa Simba na Kocha Mkuu, Fadlu David wameonesha kutoridhishwa na safu ya ushambuliaji, hivyo wameamua kutafuta mshambuliaji mwingine kabla ya dirisha kubwa la usajili kufungwa, Agosti 15.

Benchi la ufundi linataka mshambuliaji mpya atakayekuja kusaidiana na Steve Mukwala huku Fred Michael akipewa nafasi ndogo ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema viongozi wote wa Simba, akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed Dewji, wamekubaliana kuwa wanahitaji mshambuliaji mpya haraka iwezekanavyo.

Mtoa taarifa alisema kutokana na jinsi walivyoiona mechi hiyo, kama timu ingekuwa na mshambuliaji bora ingeweza kupata bao, lakini hakukuwa na kashikashi zozote langoni mwa Yanga, licha ya kiwango bora walichokionesha Simba.

"Wote wamekubaliana kuwa timu ni nzuri, lakini inakosa straika mwenye uchu wa mabao, na sasa tayari wameshaingia sokoni kumsaka mchezaji wa aina hiyo ambaye atatangazwa kabla ya dirisha dogo kumalizika, kwa maana hiyo kuna mchezaji mmoja ataondoka kumpisha, anaweza kuwa Ayoub Lakred, au Fred Michael," alisema mtoa taarifa huyo.

Hata hivyo mtoa taarifa huyo amesema kuna majina kadhaa ya wachezaji ambayo viongozi wanayo mkononi, lakini hajabahatika kuyaona na kuomba apewe muda.

"Kwa sasa sina majina ya wachezaji hao, ila nipe muda wa siku mbili tatu nitakupenyezea," alisema mtoa taarifa huyo.

Hata kwenye mechi tatu za kirafiki ilizokuwa ikicheza nchini Misri, Fadlu alikuwa akilalamikia safu yake ya ushambuliaji, akisema zinatengenezwa nafasi nyingi, lakini hazitumiwi.

Juzi baada ya mechi dhidi ya Yanga, alikiri kuwa bado kuna tatizo katika safu yake ya ushambuliaji na atalifanyia kazi kabla ya Ligi Kuu kuanza.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu hiyo, Crescentius Magori, alisema bado hawajamaliza kusajili mpaka dirisha litakapofungwa, lakini kabla ya hapo wanachama na mashabiki wategemee chochote kutokea.