Simba: Hatujakata tamaa kutinga nusu fainali CAF

By Shufaa Lyimo , Nipashe Jumapili
Published at 05:15 PM Mar 31 2024
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally.
PICHA: SIMBA SC
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally.

LICHA ya kupoteza mchezo wa kwanza ikiwa nyumbani, uongozi wa Simba umesema bado una matumaini ya kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika yanayoendelea.

Simba ilikubali kufungwa bao 1-0 na Al Ahly katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi usiku.

Akizungumza na gazeti hili mara baada ya mechi hiyo kumalizika,Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema licha ya kufungwa bao moja, lakini wachezaji wao walionyesha kiwango kizuri na walipambana.

Ahmed amesema wachezaji wao walipata nafasi nyingi za kufunga mabao lakini  walishindwa kuzitumia vyema na kupelekea kupoteza mchezo huo.

"Simba huwa hatupendi kukata tamaa mapema, tunaamini bado tuna nafasi ya kufanya vizuri katika mchezo wetu ujao wa marudiano utakaochezwa Misri, kila mmoja aliona jinsi tulivyocheza," amesema Ahmed.

Ameongeza kwa sasa wanakwenda kufanya marekebisho kwa sababu bado malengo yao ni kuingia hatua ya nusu fainali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hayajapotea.

Ameongeza mpinzani wao alipata nafasi moja na alifanikiwa kuitumia, hivyo aliondoka na ushindi akiwa ugenini.

"Tutakwenda Misri tukifahamu lolote linaweza kutokea katika mchezo wetu huo, tunaomba mashabiki na Watanzania waendelee kutuombea ili tusonge mbele, " amesema meneja huyo.

Pia amewashukuru mashabiki wao kwa  kujitokeza kwa wingi uwanjani kwa lengo la kuwaongezea hamasa wachezaji.

Al Ahly itaikaribisha Simba katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Aprili 5, mwaka huu jijini Cairo, Misri.