LIGI Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/25, ilianza kwa suluhu juzi wakati Pamba Jiji ikiwa nyumbani ilipolazimishwa matokeo hayo dhidi ya Prisons, ikiwa ni sare ya kwanza katika mechi za ufunguzi baada ya misimu minne.
Ikicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu baada ya miaka 23, Pamba Jiji ilijikuta ikishindwa kabisa kupata ushindi mbele ya mashabiki wake kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza na kuambulia kugawana pointi.
Mara ya mwisho mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara kumalizika kwa sare ilikuwa ni msimu wa 2019/20, mechi ikichezwa Agosti 24, mwaka 2019 kwenye uwanja huo huo wa CCM Kirumba kati ya Mbao FC dhidi ya Alliance, timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1, mabao yakifungwa na Paschal Liponda, huku beki wa Mbao Ibrahim Said akijifunga.
Misimu minne iliyofuata, mechi zote za ufunguzi zilitoa mshindi, Namungo ikiifunga Coastal Union bao 1-0, Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi, 2020/21, Mbeya Kwanza iliichapa Mtibwa bao 1-0, 2021/22, Uwanja wa Manungu Complex, Turiani, Morogoro, Ruvu Shooting ikishinda bao 1-0, msimu wa 2022/23 dhidi ya Ihefu, Uwanja wa Highland Estates, Mbarali, Mbeya, na msimu uliopita kwenye uwanja huo huo, Ihefu ilichapwa bao 1-0 dhidi ya Geit Gold.
Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Goran Kopunovic, licha ya kutopata ushindi ameeleza kuridhishwa na kiwango cha wachezaji wake, akisema wengi wametoka kucheza Ligi ya Championship na wamecheza dhidi ya timu kongwe ya Ligi Kuu.
"Nimeridhika, hii ni timu mpya ambayo imepanda kutoka Ligi ya Championship, kiwango cha huko na Ligi Kuu ni tofauti, nawashukuru wachezaji wangu wamepambana na timu kongwe, yenye wachezaji wazuri ya Prisons," alisema kocha huyo raia wa Serbia.
Hata hivyo kocha huyo alilalamika kikosi chake kilikosa ushindi kutokana na kupangua kikosi muda mchache kabla ya mechi hiyo haijaanza.
Mserbia huyo alisema alilazimika kuwaondoa wachezaji wake watano waliokuwa katika kikosi cha kwanza baada ya kubainika usajili wao ulikuwa haujakamilika.
Naye Kocha Msaidizi, Shaaban Kazumba, alisema kwa kiasi kikubwa suluhu hiyo imepatikana kwa sababu ya kufahamiana.
Pamba Jiji wanamfahamu Kocha, Mbwana Makata kwa sababu aliifundisha timu yao, na yeye anaifahamu, hii imechangia sana, tulianza mechi ili tupate mabao ya mapema, tukapoteza nafasi nne za wazi, kipindi cha kwanza eneo letu la katikati halikuwa zuri ilibidi tufanye mabadiliko, kipindi cha pili pia tukatengeneza nafasi tukashinda kuzitumia, timu yetu ina mapungufu madogomadogo ambayo tunakwenda kuyarekebisha," alisema Kazumba.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED