Sababu dabi, Simba, Yanga kutokuwa na VAR hizi hapa

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 10:22 AM Aug 11 2024
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Almasi Kasongo
Picha: Mtandao
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Almasi Kasongo

BODI ya Ligi imesema hakutakuwa na video ya kusaidia waamuzi VAR katika mechi za mwanzo wa Ligi Kuu mpaka hapo baadaye kutokana na marefa wanaotakiwa kuifanya kazi hiyo kuwa kwenye mafunzo kwa sasa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Almasi Kasongo, alisema hayo jijini Dar es Salaam, na kuzima malalamiko ya baadhi ya mashabiki wa soka nchini waliokuwa wanahoji kutokuwepo kwa VAR katika mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga uliochezwa Alhamisi iliyopita, Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni nusu fainali ya Ngao ya Jamii.

"Kwa sasa tunawajengea uwezo waamuzi wetu wataokuwa kwenye VAR kama tulivyoelekezwa na CAF na FIFA, na watajifunza mpaka wenyewe waje kujiridhisha kuwa wameiva kuwa sehemu ya VAR, baada ya hapo sasa tutaomba kibali cha kuitumia kwenye Ligi yetu," alisema Kasongo na kuongeza.

"Kwa hiyo, michezo ya awali hatutokuwa na VAR mpaka mchakato huo umalizike," alisema.

Hivi karibuni, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), liliipa Shirikisho la Soka Tanzania mitambo ya VAR, ambayo imefungwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku wadhamini waliopewa tenda ya kuonyesha mipira nao wakiahidi kuwa na VAR inayohamishika 'Mobile VAR.'

Baada ya mechi ya Alhamisi, ambayo Yanga ilishinda bao 1-0, baadhi ya mashabiki walilalamika kutotumika kwa VAR, na hiyo ilitokana na baadhi ya matukio tata ambayo mwamuzi Elly Sasii na wasaidizi wake walionekana kushindwa kuyaamua kwa usahihi.