KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Maxi Nzengeli, amesema amefurahia kufunga bao la kwanza la msimu kwa timu yake pamoja na kufikia rekodi iliyowahi kuwekwa na Wakongomani wenzake, Heritier Makambo na Fiston Mayele miaka ya nyuma, imefahamika.
Nzengeli anakuwa Mkongomani watatu kufunga mabao ya kwanza ya msimu kwa Yanga, baada ya kufunga bao la kwanza katika ushindi wa magoli 2-0 ambao waliupata ugenini dhidi ya Kagera Sugar, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, mkoani Kagera Alhamisi iliyopita.
Akizungumza na gazeti hili jana, Nzengeli alisema awali hakufahamu hilo kabla ya kuambiwa na watu wa kitengo cha habari na mawasiliano cha klabu hiyo.
"Nimefurahi sana kwa sababu nimekuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao msimu huu katika kikosi chetu, lakini pia nimeambiwa nimefuata nyayo za Wakongomani wenzangu, kaka zangu, Makambo na Mayele ambao waliwahi kufanya kama mimi, kwa maana hiyo nimeendelea kupeperusha vyema bendera ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo hapa Tanzania," alisema mchezaji huyo.
Katika mchezo huo, Yanga ilishinda mabao 2-0, goli la pili likiwekwa wavuni na Mtanzania Clement Mzize, dakika mbili kabla ya mechi kumalizika.
Msimu wa Ligi Kuu 2018/2019, Makambo alikuwa mchezaji wa kwanza wa Yanga kufunga bao la msimu, akipachika bao katika mechi iliyofanyika Agosti 23, mwaka 2018, timu hiyo ikicheza dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Makambo alifunga bao dakika ya 30, mechi iliyoisha kwa Yanga kushinda mabao 2-1, goli la pili likifungwa na beki, Kelvin Yondani kwa mkwaju wa penalti wakati lile la kufutia machozi la Mtibwa Sugar likiwekwa wavuni na Haruna Chanongo.
Kwa upande wa Mayele, yeye alifunga bao la kufungulia msimu wa Ligi Kuu 2022/23 katika mechi ambayo Yanga ilicheza dhidi ya Polisi Tanzania, Agosti 16, mwaka 2022 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, mechi hiyo iliisha kwa Yanga kupata ushindi wa mabao 2-1, Mayele akitangulia dakika ya 41, kabla ya Bakari Mwamnyeto kufunga la pili, Salum Kipemba akifunga bao la kufutia machozi kwa wenyeji.
Naye nahodha msaidizi, Dickson Job, ambaye msimu uliopita ndiye aliyefunga bao la kwanza kwa timu hiyo, ameeleza kufurahishwa kwake kuchangia bao la Nzengeli.
"Msimu uliopita mimi nilifunga bao la kwanza, msimu huu ilikuwa bado kidogo nianze na 'asisti', lakini nimechangia bao la kwanza. Ule mpira mimi ndiye niliyempa Maxi, sasa badala ya kwenda kufunga, yeye akampasia kwanza Stephane Aziz Ki, ndipo alipoharibu, halafu akamrudishia mwenyewe akaenda kufunga bao," alisema Job huku akicheka.
Msimu uliopita, Job alifunga bao la kufungulia msimu, Agosti 23 mwaka jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, alipopachika bao dakika ya 16, Yanga ikicheza dhidi ya KMC, na kuibuka kidedea kwa mabao 5-0.
Mara ya mwisho Yanga kupoteza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara ilikuwa ni Septemba 20, 2014 ilipofungwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani, Morogoro dhidi wenyeji Mtibwa Sugar, mabao yaliyofungwa na Mussa Hassan 'Mgosi' na Ame Ally.
Simba ndio vinara wa ligi hiyo yenye timu 16, akiwa na pointi sita baada ya kushinda mechi zote mbili walizocheza sawa na Singida Fountain Gate huku Mashujaa FC ya Kigoma ikiwa kwenye nafasi ya tatu na pointi zake nne kibindoni wakati Yanga inafuatia ikiwa na pointi tatu.
Fountain Gate ya Singida iliyopanda daraja msimu huu inafuatia katika msimamo huo ikiwa na pointi tatu sawa na Tabora United ya mkoani Tabora.
Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kupisha kalenda ya kimataifa ambapo hapa nchini Taifa Stars itawakaribisha Ethiopia katika mechi ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika itakayochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED