WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damasi Ndumbaro anatarajiwa kuzindua mashindano ya kwanza ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali John Mkunda Agosti 19, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano hayo, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy, alisema mashindano hayo ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
“Mashindano haya ni wazo la CDF, lengo lake ni kuhuisha sanaa na utamaduni nchini, akaona jeshi lina uwezo wa kufufua sanaa hiyo mpaka kufikia kimataifa, zamani wakati tuko shule ya msingi tulipata kuona sanaa mbalimbali ikiwamo mazingaombwe, sarakasi, ngoma za asili zetu na nyingine nyingi lakini sasa havipo tena.
“Kupitia mashindano haya kwa mara ya kwanza mwaka huu, yatashirikisha vikundi vya utamaduni na bendi za JWTZ, yataendelea kufanyika kila mwaka na 2025 tutaalika vyombo vingine vya ulinzi na usalama ikiwamo Jeshi la Magereza, Uhamiaji na Polisi pamoja na kuongeza fani nyingine za sanaa.
“Tunawaita Watanzania Wote waje kushuhudia burudani hizo zitakazozinduliwa hapa Msasani Klabu, hakutakuwa na kiingilio ni burudani kuelekea shamrashamra za miaka 60 ambazo kilele chake ni Septemba Mosi”alisema Meja Jenerali Mkeremy.
Meja Jenerali Mkeremy alisema Kamati yake itaungana na majaji watatu kutoka Basata watakaoshauri na kuboresha mashindano hayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED