JKT Tanzania yajipanga kumpa unahodha Bocco

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 01:16 PM Jun 30 2024
Straika mkongwe nchini, John Bocco.
Picha: Maktaba
Straika mkongwe nchini, John Bocco.

KAMA mambo yataenda kama yalivyopangwa, JKT Tanzania itamtangaza straika mkongwe nchini, John Bocco, kuwa mchezaji na nahodha wa timu hiyo kuelekea msimu mpya wa mashindano wa mwaka 2024/2025.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema, licha ya nahodha huyo wa zamani wa Simba kupewa kazi ya kukinoa kikosi cha vijana chini ya miaka 17, mabosi wa JKT Tanzania wamekuwa wakimshawishi arejee uwanjani na wanaamini bado ana uwezo mkubwa.

"Tunamhitaji Bocco, katika tathmini yetu tumegundua hapa Tanzania huwezi kumpata straika kama yeye, japo ana umri mkubwa, lakini ana uwezo kuliko washambuliaji wengi vijana tulionao. Shida yetu kubwa msimu uliopita ilikuwa ni straika.

Tukiangalia hatuwezi kusajili straika wa kigeni, wa hapa ndiyo hawa msimu mzima ana mabao matano tu, tukaona bora twende kwa Bocco ambaye kwa misimu yote aliyocheza Ligi Kuu, alikuwa akipiga mabao yasiyopungua 10, tumeona tumrudishe uwanjani," amesema mtoa habari wetu.

Kimeongeza chanzo hicho kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za mazungumzo huku wakiwa wanasubiria jibu chanya kutoka kwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Azam FC.

"Mambo yanakwenda vizuri, tuko katika hatua za mwisho kabisa, baada ya hapo tutamtambulisha kama mchezaji na nahodha wa kikosi chetu, tutampa mkataba wa mwaka mmoja, kama akifanya vyema mpaka nusu msimu, tunamwongeza tena mwaka mmoja," kimesema chanzo hicho.

Bocco aliyeichezea Simba kwa misimu saba kuanzia mwaka 2017, alikuwa mchezaji wa kwanza kutangazwa kuachwa na Wekundu wa Msimbazi lakini akiwa amepewa jukumu jipya klabuni hapo.