Coastal Union yafuata makali Pemba

By Shufaa Lyimo , Nipashe Jumapili
Published at 10:34 AM Aug 04 2024
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Abbas El Sabri
Picha: Mtandao
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Abbas El Sabri

KIKOSI cha Coastal Union kimehamisha kambi yake kutoka Unguja na kuelekea Pemba kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC utakaochezwa Agosti 8 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Akizungumza na Nipashe jana, Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Abbas El Sabri alisema wanahamisha kambi hiyo kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo. 

"Leo (jana) tumehamishia kambi yetu Pemba kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wetu huo ambao unatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa, lengo ni kupata ushindi na kusonga mbele kuingia kwenye fainali," alisema El Sabri. 

Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, David Ouma, alisema michezo minne ya kirafiki waliyoicheza visiwani humo imemsaidia kutengeneza muunganiko wa timu na kutoa taswira halisi pindi msimu ujao utakapokuwa tumeanza. 

Alisema malengo yake ni kushinda kwenye mchezo huo wa Ngao ya Jamii na anashukuru mpaka sasa hana mchezaji yeyote ambaye ni majeruhi. 

"Michezo ya kirafiki tuliyoicheza imenisaidia kuimarisha zaidi kikosi changu ambacho ninaamini kitafanya vizuri katika mchezo huo pamoja na ile ya msimu ujao wa Ligi Kuu itakayoanza Agosti 16, mwaka huu," alisema Ouma. 

Mpaka sasa timu hiyo imecheza michezo minne ya kirafiki ambapo mchezo wa kwanza walicheza na Tekeleza FC na kufanikiwa kushinda bao 1-0, mchezo wa pili walicheza na Kombaini na kushinda mabao 8-0, pia walicheza na Jamhuri na kufanikiwa kuichapa mabao 4-0 kabla ya kucheza na Chipukizi na kuibuka na ushindi wa mabao 4-0.