KIKOSI cha Azam FC kinatarajia kuwakaribisha APR kutoka Rwanda katika mechi ya kwanza ya hatua ya awali ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Kocha Mkuu wa Azam FC, Bruno Ferry, alisema jana jijini mechi hiyo itakuwa na ushindani kwa sababu kila timu imejiandaa kusaka ushindi.
Ferry alisema amekiandaa vyema kikosi chake ili kuhakikisha wanaanza vizuri michuano hiyo na kujiweka katika nafasi salama ya kusonga mbele.
Alisema timu yake ilistahili kufuzu mashindano hayo na sasa wanachotaka kukionyesha ni ubora wao pia katika michuano hiyo ya kimataifa inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
"Michuano hii ni muhimu sana kwetu kwa sababu kama tupo hapa leo, basi ni kwa sababu tulifanya kazi kubwa msimu uliopita kuipata tiketi hii. Ilikuwa ni kazi kubwa kutoka kwa wachezaji, benchi la ufundi na watu wote wanaoizungumza timu, hivyo tunaweza kusema tumestahili kuwa hapa kucheza michuano hii," alisema Ferry.
Naye beki wa timu hiyo, Cheikh Sidibe, alisema wako tayari kwa mechi hiyo na wanatarajia kupata ushindi.
"Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mechi hiyo na kila mechi iliyoko mbele yetu, tumejipanga na tuko tayari kwa ajili ya kupata ushindi katika mechi ya Jumapili, Inshaa-Allah tutashinda," alisema beki huyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED