Wachezaji wa Gofu kuchuana Julai Dar

By Shufaa Lyimo , Nipashe Jumapili
Published at 08:58 AM Jun 23 2024
Wachezaji wa Gofu  kuchuana Julai Dar.
Picha: Mtandao
Wachezaji wa Gofu kuchuana Julai Dar.

MASHINDANO ya wazi ya gofu yamepangwa kufanyika Julai 5 hadi 7, mwaka huu kwenye viwanja vya Klabu ya Lugalo, Dar es Salaam imeelezwa.

Akizungumza jijini jana, Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, Brigedia Jenerali Mstaafu, Michael Luwongo, alisema shindano hilo litashirikisha klabu mbalimbali kutoka Tanzania Bara.

Luwongo alisema lengo la mashindano hayo ni kuwafanya wachezaji wapate nafasi ya kuonyesha viwango vyao lakini pia kuboresha mahusiano baina ya watu mbalimbali watakaoshiriki.

"Shindano hili litakuwa la aina yake kwa sababu mpaka sasa idadi kubwa ya washiriki wameanza kujiandikisha ili kuonyesha nia ya ushiriki wao, ninaamini kila klabu itaonyesha upinzani mkubwa," alisema Luwongo. 

Alisema mashindano hayo yatakuwa na makundi matatu ambayo ni watoto, wanawake na wachezaji wakongwe.

Naye Rais wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Gilman Kasiga, alisema wachezaji watakaofanya vizuri watapata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa huku akiwashukuru wadau waliojitokeza katika kusaidia maandalizi.

"Mchezo wa gofu kwa sasa umeshika kasi tofauti na miaka iliyopita, kuna idadi kubwa ya Watanzania wanajiunga, tunaamini sisi TGU pia itatusaidia kupata wachezaji watakaoiwakilisha nchi katika mashindano mbalimbali yaliyoko mbele yetu," Kasiga alisema.