BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaendelea na mkutano wake wa 18 jijini Dodoma, huku likiwa tayari limepitisha miswada mitatu nyeti iliyokuwa ikivuta hisia za Watanzania wengi. Miswada hiyo ni ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani; Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Sheria ya Vyama vya Siasa.
Kabla ya kupitishwa kwa miswada hiyo, kulikuwa na mijadala mikali iliyotolewa na wabunge iliyofanya serikali kukubaliana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala ambayo ilipokea maoni na kuyachakata kabla ya kuwasilishwa bungeni. Miongoni mwa mambo yaliyokubaliwa ni mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa NEC kupitia katika usaili kama wajumbe wengine wa tume kabla ya majina yao kuwasilishwa kwa Rais kwa kuridhiwa na hatimaye kuteuliwa.
Pamoja na mjadala wa miswada hiyo na shughuli zingine za Bunge kama maswali ya kawaida na yale yanayoelekezwa kwa Waziri Mkuu, kuna jambo lililovuta hisia na mijadala kutoka kwa wadau wa siasa. Jambo hilo ni Mbunge wa Momba (CCM), Condester Sichalwe, kutinga na video fupi bungeni inayoonesha baadhi ya wananchi wa jimbo hilo wanavyopata adha ya maji safi na salama, hivyo kutumia maji machafu yanayopatikana kwenye visima vya asili.
Mbunge Sichalwe alisema amefikia hatua hiyo baada ya wizara ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria iliyoahidi kuchimba visima vya dharura lakini hadi sasa hakuna hata tone la maji. Wizara ilieleza Aprili, mwaka jana kuwa Sh. bilioni 9.5 ziliahidiwa kumaliza tatizo la maji katika jimbo hilo lakini hakuna utekelezaji wowote uliofanyika.
Kutokana na kutokutekelezwa kwa ahadi hiyo, alisema anaogopa kwenda jimboni kuwaeleza wananchi wake kwa kuwa ataonekana tapeli. Kwa maneno mengine, wananchi watakosa imani naye, hali itakayomfanya akose kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Hata hivyo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alipopewa nafasi, alijibu kwamba kitendo hicho kinaweza kuwakatisha tamaa watendaji kwa kuwa kazi inafanyika katika kutatua kero hiyo jimbo la Momba.
Ni wazi kwamba mbunge alikuwa akiwakilisha kilio cha wananchi wake lakini jambo la kujiuliza ni je, katika eneo hilo hakuna Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) ambao umepewa jukumu la kutekeleza miradi ya maji? Pia ni hatua gani iliyochukuliwa katika ngazi ya halmashauri kwa maana ya baraza la madiwani katika kutatua kero hiyo.
Kama alivyosema mbunge kwamba suala hilo lilifikishwa bungeni mwaka jana, lakini kulikuwa na ulazima gani wa kulirejesha ilhali Waziri anasema katika kuanza kwa kazi hiyo, serikali ilishatoa Sh. milioni 500 kwa ajili ya kuanza kutekeleza miradi hiyo?
Licha ya kulalamika, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi, awali alijibu kwamba jimbo hilo lina jumla vijiji 72 na mpaka sasa vijiji 30 vinapata huduma ya maji safi na salama kupitia miradi 18 ya maji ya bomba. Sambamba na vijiji hivyo, ilielezwa kuwa kuna utekelezaji wa miradi mingine ya maji katika vijiji 12 ndani ya Momba.
Hatua aliyochukua mbunge ni nzuri na ina mashiko lakini ni vyema wabunge wakajua nini yawapasayo kufanya wawapo bungeni na yale wakiwa katika halmashauri. Ni dhahiri kwamba Sichalwe angepata majibu kama angefuatilia ngazi ya wilaya kupitia RUWASA vinginevyo, kinachoonekana alikuwa akihofia kupoteza ugali wake ifikapo 2025 kwamba hakuna kitu alichokifanya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED