LEO ni miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Wananchi wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla, wanakumbuka Mapinduzi hayo matukufu yaliyoung’oa utawala wa Sultan wa Oman aliyetawala visiwa hivyo na kuwezesha wananchi kujitawala kutoka katika makucha ya wakoloni.
Januari 12, 1964 wananchi wa Zanzibar baada ya kuchoshwa na kufanyiwa ghiliba za kila aina wakati wa harakati za ukombozi na hatimaye kupata uhuru kamili, waliamua kwa nguvu moja kwa kutumia marungu na mapanga, kujikomboa kutoka katika vifungo hivyo vya kutawaliwa na wageni.
Mapinduzi hayo yanakumbusha historia ya visiwa vya Zanzibar, yaani Unguja na Pemba, katika kujikomboa kwao kutoka katika kukandamizwa na kuwa wanyonge ndani ya taifa lao. Kazi hiyo yenye kutukuka, iliyofanikisha kufikiwa kwa azma hiyo, ilifanywa na wanyonge- wakulima, wavuvi na wakwezi wakiongozwa na viongozi wao chini ya Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar.
Kabla ya Mapinduzi hayo matukufu, wananchi hao walinyanyaswa na kubaguliwa katika mambo mbalimbali kama vile elimu, afya na huduma. Kulikuwa na matabaka katika utoaji wa huduma na wazawa ambao ni Waafrika na wenyeji halisi wa Zanzibar, walitengwa na kuonekana kuwa ni daraja duni. Hiyo ndiyo moja ya sababu zilizofanya wazawa wajikusanye na hatimaye kufanya mapinduzi hayo matukufu yaliyoleta uhuru ndani ya visiwa hivyo.
Baada ya Mapinduzi hayo, Mzee Karume aliondoa matabaka na ubaguzi uliokuwa umetamalaki na kuweka bayana kuwa watu wote ni sawa. Kwa maana hiyo, mapinduzi hayo jambo la kwanza lililofanikiwa ni kuondoa ubaguzi baina ya wazungu, waasia na waafrika ndiyo maana iliamriwa kama mwafrika amemwona muasia au mzungu kuwa ni mzuri, basi aoe.
Waafrika kabla ya Mapinduzi hayo walitengwa na kukosa makazi bora tofauti na watu wa rangi zingine, hivyo zikafanyika jitihada za kuwawezesha wazawa kuwa na nyumba za kuishi. Matokeo ya mpango huo ni kuwapo maghorofa ya Michenzani, Unguja na mengine kisiwani Pemba.
Tangu kufanyika kwa Mapinduzi hayo miaka 61 iliyopita, kumeshuhudiwa mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii visiwani Zanzibar. Katika awamu zote za uongozi, kumekuwa na maendeleo makubwa katika masuala mbalimbali. Mabadiliko hayo yamesababisha wananchi kuwa na hali nzuri za kiuchumi. Kumekuwa na maendeleo ya miundombinu ya uchukuzi kama vile bandari, barabara na viwanja vya ndege ambayo imechochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi.
Sekta ya utalii imekuwa kichocheo kikubwa kwa maendeleo ya uchumi wa Zanzibar. Watu kutoka mataifa mbalimbali wamekuwa wakifika katika visiwa hivyo na kutembelea fukwe mwanana za Bahari ya Hindi zilizoko huko pamoja na vivutio mbalimbali na maeneo ya kale.
Hatua hiyo pia imevutia wawekezaji mbalimbali kujenga hoteli mbalimbali za kitalii kwenye visiwa vidogo na maeneo ya miji mikubwa. Ujenzi huo wa hoteli umechangia pato la taifa na kuboresha sekta ya utalii kwa ujumla.
Pia imeshuhudiwa uboreshaji wa huduma za afya na elimu Zanzibar mwaka hadi mwaka na sasa kuna mafanikio makubwa katika sekta hizo kulinganisha na kabla na baada ya Mapinduzi. Hospitali kubwa zimejengwa na huduma kuboreshwa huku katika elimu, shule nyingi kuanzia za awali mpaka sekondari zimejengwa na kuna wasomi wengi wa ngazi ya shahada hadi ya uzamivu kulinganisha na awali.
Aidha, kwa sasa kuna sera ya uchumi wa buluu ambao unashajihisha maendeleo endelevu ya kiuchumi kwa watu wa Zanzibar kupitia bahari kama vile uvuvi, kilimo cha mwani, utatifi na utafutaji wa gesi na mafuta. Kwa hakika Zanzibar ya sasa imenoga na Mapinduzi ambayo ni chanzo cha yote, yadumishwe na kuenziwa kwa vitendo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED