Kasumba vijana kuhusu ajira mikoa ya pembezoni imepitwa na wakati

Nipashe Jumapili
Published at 07:44 AM Nov 24 2024
Ajira.
Picha:Mtandao
Ajira.

KWA miaka mingi, kumekuwa na kasumba iliyojengeka kwa watumishi wa umma au wafanyakazi wa sekta binafsi kukataa kwenda katika mikoa ya pembezoni pindi wanapopangiwa kwenda huko.

Mikoa hiyo ni Rukwa, Kigoma, Katavi, Mtwara na Lindi. Hali hiyo pia ilizikumba baadhi ya wilaya zilizokuwa na tatizo la miundombinu au mawasiliano kama vile Simanjiro na Kiteto mkoani Manyara na Ukerewe mkoani Mwanza 

Licha ya kubadilika kwa mambo ikiwamo kuboreshwa kwa miundombinu katika mikoa hiyo pamoja na kuibuliwa kwa fursa mbalimbali, bado wafanyakazi na watumishi wamekuwa wakikataa kuripoti na kufanya kazi katika maeneo hayo.  

Awali, waliokuwa wakipangiwa katika mikoa hiyo miaka ya 1990 na kurudi nyuma, walikuwa na dhana kwamba wanakomolewa, hivyo kushindwa kwenda na kuamua kuacha kazi. Baadhi yao walikuwa wakiripoti kisha kuomba kuhamishwa kwa kutoa sababu mbalimbali kama vile za kifamilia au ugumu wa mazingira ya kufanya kazi.  

Hata sasa, licha ya kuboreshwa kwa mazingira, hali hiyo bado inaendelea kama alivyoshangazwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu. Naibu Waziri alishangaa  baada ya kubaini kuwa kuna idadi ndogo ya waombaji wa nafasi za kazi  kada ya afya waliokuwa katika mikoa ya Kigoma,  Katavi, Lindi na Mtwara.  

Hali hiyo ni tofauti na mikoa mingine kama vile Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma ambayo ina idadi kubwa ya waombaji kulinganisha na  uhitaji. Wanaoomba kazi katika mikoa hiyo ni wachache kulinganisha na mikoa mingine. Utaratibu wa watu kuomba kazi katika mikoa wanayotaka kufanyia kazi umeandaliwa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma badala ya ule uliozoeleka wa watu kuomba kazi na hatimaye waliofaulu usaili kupangiwa vituo.  

Juni, mwaka huu, sekretarieti hiyo ilitangaza nafasi za kazi 9,483 za kada ya afya na kila mwombaji alitakiwa kuomba ajira katika mkoa ambao atafanya kazi endapo atafanikiwa kupita kwenye usaili. 

Waziri Sangu alitolea mfano wa mkoa wa Kigoma, ambao mahitaji halisi ya waliotakiwa kuajiriwa katika kada ya afya yalikuwa watumishi 400 lakini waombaji walikuwa hawazidi 200. Hali hiyo pia ilikuwa katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Katavi ambako pia idadi ikiwa ndogo kulinganisha na uhitaji. 

Kutokana na kuwapo kwa hali hiyo, Sangu alishangazwa na uwapo wa tatizo kubwa la ajira kwa vijana nchini lakini wanashindwa kuchangamkia fursa zinapojitokeza kwa kuendekeza kasumba iliyojengeka miaka nenda rudi kwamba mikoa hiyo ya pembezoni ina mazingira magumu ya kufanya kazi na ukosefu wa baadhi ya huduma.  

Licha ya kuwapo kwa hali hiyo, Naibu Waziri pia alishangazwa na tabia ya baadhi ya watumishi wanaopangiwa katika mikoa hiyo kuomba uhamisho muda mfupi baada ya kuripoti. Hali hiyo imeiamsha serikali na kuonya kuwa haitawavumilia watumishi wa namna hiyo na kusisitiza kuwa ni lazima wafanye kazi kwa miaka mitatu na kuendelea ndipo waombe uhamisho.  

Kuendelea kuwapo kwa kasumba hiyo ni jambo la kushangaza kwa sababu serikali imeboresha mazingira ya kufanya kazi katika maeneo yote ya nchi ikiwamo mikoa ya pembezoni ambayo awali ilikuwa vigumu kupatikana kwa huduma mbalimbali. Kama ni miundombinu, hivi sasa hakuna mkoa ambao haujaunganishwa na barabara ya lami. Pia kuwapo kwa miundombinu kumewezesha kuwapo kwa huduma mbalimbali kila kona ya nchi.  

Ni vyema kwa vijana wanaoomba ajira, wakaachana na kasumba hiyo ambayo imejengeka katika fikra zao. Kama wahenga wasemavyo kambi popote, ni vyema vijana wanaosaka ajira wakachangamkia mikoa hiyo kwa sababu kuna uwezekano wa kupata kazi kama ilivyobainishwa na Naibu Waziri Sangu.