MAGONJWA yasiyoambukiza katika miaka ya karibuni, yameelezwa kuwa yanachangia kwa kiasi kikubwa vifo vya watu na hata kusababisha kupungua kwa nguvu kazi katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo. Miongoni mwa magonjwa yanayotajwa ni shinikizo la juu la damu, kisukari na maradhi ya moyo.
Sababu kubwa zinazotajwa kuwa chanzo cha maradhi hayo ni ulaji wa vyakula bila mpangilio hasa vile vyenye mafuta kwa wingi, mtindo wa maisha, kutokufanya mazoezi na kutozingatia ushauri wa wataalamu wa afya.
Shikinizo la damu na magonjwa ya moyo, kwa mfano, taarifa za kitabibu zinabainisha kuwa yamekuwa yakisababisha vifo vya ghafla watu wakiwa wamekaa, wakifanya kazi au wakiwa wamelala. Pia maradhi hayo yameelezwa kuwa husababisha vifo vya watu hata wakiwa kazika michezo au mazoezi kutokana na kutokupima hali zao kabla ya kuanza shughuli hizo.
Ushuhuda mmojawapo ni wa juzi baada ya Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Mlima Ngaile, kufariki dunia wakati akishiriki mbio za Wiloles Foundation Marathon 2024. Akiwa mmoja wa viongozi waandamizi, alishiriki mbio hizo akijumuika na wenzake kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto waliozaliwa kabla ya muda (njiti) katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Ruvuma ya Songea (HOMSO).
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Songea, Wiliam Kapenjama, meneja huyo alifariki juzi saa 3:00 asubuhi. Meneja huyo, viongozi na washiriki wengine, walifika katika viwanja vya michezo vya Majimaji na kujisajili kisha wakaanza kukimbia umbali wa kilometa tano. Wakiwa katika mbio hizo, Ngaile aliwapita washiriki wenzake na muda mfupi kidogo alianguka na kupoteza fahamu kabla ya kubainika kuwa amefariki dunia baada ya kufikishwa hospitalini.
Kifo cha meneja huyo wa TANROADS ni kimojawapo ya vile vingi ambavyo vimekuwa vikitokea kutokana na maradhi yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu. Licha ya kwamba ni wachache wanaobainika na kutangazwa, vifo vya namna hiyo ni vingi na kwa kiasi kikubwa vimekuwa vikigharimu maisha ya watu wengi ambao ni nguvu kazi ya taifa.
Kutokana na ongezeko la vifo vya namna hiyo na vile vitokanavyo na maradhi ya moyo na kisukari, viongozi na wataalamu wa afya, mara kwa mara wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa watu kupima afya zao ili kujua kama wana maradhi hayo ili wapate ushauri na tiba kabla tatizo halijawa kubwa.
Pamoja na ushauri huo, madaktari na madaktari bingwa katika tiba, pia wamekuwa wakiwashauri watu kupima afya zao kabla ya kuanza kufanya mazoezi na kwamba hata kama hawana matatizo kama hayo, wafuate kanuni na taratibu ili kuwaepusha na madhara yanayoweza kujitokeza ghafla na hata kupoteza maisha.
Ni ukweli usiopingika kwamba hivi sasa katika miji mikubwa kama vile Dar es Salaam, kumekuwa na mwitikio mkubwa wa watu kufanya mazoezi ya kukimbia au kwenye maeneo maalum, maarufu kama ‘Gym’. Licha ya kuwapo kwa mwitikio huo, je, wanafuata ushauri wa madaktari juu ya kupima afya kabla ya kuanza kufanya?
Ni wakati mwafaka sasa kwa Watanzania kuwa mstari wa mbele katika upimaji wa afya ili kujikinga na matatizo yanayoweza kuzuilika ikiwamo vifo vinavyotokana na maradhi ya moyo na shinikizo la damu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED