VUGUVUGU la uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu na uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwakani, limeanza kushika kasi huku kukiwa na matamko mbalimbali ya viongozi wa vyama vya siasa.
Mbali na matamko hayo yenye viashiria vya kupanda kwa joto hilo, pia baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wamekuwa wakifanya ziara katika mikoa mbalimbali kwa lengo la kuvijenga vyama na kutafuta uungwaji mkono.
Katika ziara za viongozi wa vyama hivyo, Chama Cha Mapinduzi ambacho kwa sasa kinashika dola, wajumbe wa sekretarieti wamefanya ziara mara kadhaa kwa kile wanachokiita kukagua uhai wa chama na kusisitiza maendeleo.
Hivi karibuni sekretarieti hiyo ilifanya ziara takriban mikoa yote na wajumbe wake kuweka misimamo ya chama katika masuala mbalimbali huku wakisisitiza kuwa nia ya chama hicho ni kuendelea kushika dola na kuendelea kuongoza nchi kutokana na imani waliyo nayo Watanzania kwao.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeendelea kuendesha siasa zake kwa kufanya maandamano katika kanda mbalimbali za kichama huku ajenda kubwa zikiwa kikokotoo cha mafao ambacho kimekuwa kikilalamikiwa na watumishi, kupanda kwa gharama za maisha na bidhaa ikiwamo sukari.
Licha ya ziara na matukio hayo ya kisiasa, kumekuwa na kauli na matamko kutoka kwa baadhi ya viongozi ambayo yamekuwa na viashiria vya kwenda kinyume cha misingi ya kidemokrasia na hali ya amani na utulivu nchini.
Mmoja wa viongozi wa CCM mkoani Kagera, kwa mfano alisema watawapoteza baadhi ya wapinzani ambao wamekuwa wakikosoa serikali na polisi wasiwatafute. Mwingine naye akasema Watanzania wasio wanachama wa CCM ni wasaliti na wamemwasi Mungu.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CCM, alisimama na kusema Tanzania ni ya Watanzania wote bila kujali itikadi zao.
Viongozi wengine wa vyama vya upinzani ambavyo vinaendesha siasa kama ilivyo CCM, nao wamekuwa wakitoa kauli mbalimbali ambazo zina ukakasi kama vile kuwataja viongozi wanaosababisha kupanda kwa bei ya sukari na bidhaa kwa madai kwamba wanawalazimisha wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa hizo nje ya nchi kuongeza fedha kidogo kwa madai ni maagizo kutoka juu.
Chama cha ACT Wazalendo nacho kimekuwa kikitoa kauli mbalimbali ikiwamo jana kwamba katu hakitakubali kuhujumiwa katika uchaguzi mkuu mkuu utakaofanyika mwakani, hasa ule wa Zanzibar.
Matamko hayo, yanakinzana na dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kuendesha siasa kistaarabu na kwamba kila chama na wafuasi wake kiko huru kufanya mikutano na hata maandamano ilimradi visivunje sheria. Rais pia amekuwa akisisitiza maelewano, maridhiano na ujenzi upya wa taifa kupitia kile alichokiita R4.
Juzi, mathalan, Tanzania ilikuwa inatimiza miaka 60 tangu kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uliozaa taifa la Tanzania huku viongozi wakuu wakihimiza Watanzania kuendelea kuulinda Muungano kwa ustawi wa taifa. Ustawi wa Muungano huo umetokana na kuwapo kwa amani, utulivu, umoja na mshikamano ambavyo ni nguzo katika kudumu kwake.
Ni dhahiri kwamba hakuna anayezuwia kufanya siasa katika utawala wa sasa lakini kinachosisitizwa ni kuendesha siasa za kistaarabu ambazo haziwaumizi wengine kwa njia ya matusi, hila na ghiliba. Serikali imeweka wazi suala hili, hivyo hakuna haja ya kusimama majukwaani na kutukana watu au kutoa kauli za vitisho.
Huo si utamaduni wa Watanzania walioishi kwa amani na upendo bila kujali imani wala itikadi zao.
Ni vyema kila mtu anayefanya siasa, afanye huku akizingatia kwamba Tanzania ni ya watu wote walioko katika ardhi hii na hakuna mwenye hatimiliki ambaye anajiona ana uhuru wa kutoa kauli za matusi, vitisho na kashfa dhidi ya viongozi na Watanzania wengine. Ustaarabu ndiyo silaha yetu na tuudumishe kwa amani na umoja wa taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED