KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, ametatua kero 60 za wananchi wa Longido na Karatu na kuunda kamati kila wilaya ya ufuatiliaji ili kila mwananchi aliyewasilisha jambo lake lipatiwe ufumbuzi wa kudumu.
Usikilizaji na utatuzi wa kero za wananchi unaofanywa na kiongozi huyo kila anapokwenda, hutanguliza maofisa wa chama kusikiliza wananchi na kurekodi kero zao ambazo kupitia mkutano wake wa hadhara kila jioni husomwa na mtaalam hueleza hatua zilizochukuliwa.
Miongoni mwa kero ambazo zimejirudia katika mikutano yake ni zinazohusu ukosefu wa maji na kukatikatika kwa umeme, hali inayowafanya wananchi kushindwa kufanya shughuli za uzalishaji.
Akiwa Longido wanachama wa CCM, walisema kuna mradi wa maji wa muda mrefu wa kutoa maji Mto Simba ambao bado haujakamilika, huku Mji wa Longido ukiwa na shida kubwa ya huduma hiyo muhimu.
Suala hilo lilijitokeza pia, Kilimahewa Kata ya Mundarara, kwenye mkutano wa hadhara ambapo kila kiongozi wa chama na mbunge walivyopanda jukwaani, walieleza kero kubwa ni ukosefu wa maji na kumwomba kuitatua.
Kwenye mkutano wa hadhara Karatu mjini, kila aliyepanda jukwaani, alitaja kero hiyo kuwa imetokana na mafuriko yaliyoharibu miundombinu.
"Katika mji wetu wa Karatu kuna tatizo kubwa la maji baada ya miundombinu kuharibiwa na mafuriko. Wananchi unaowaona hapa shida yao kubwa ni maji,” alisema Mbunge wa Karatu, Daniel Awack, huku akishangiliwa na wananchi.
Kutokana na kilio hicho, Makalla alimpigia simu mara tatu Waziri wa Maji, Juma Aweso, akiwa kwenye kikao na viongozi wa chama, Mundarara na Karatu ambaye pamoja na kuahidi kushughulikia, alisema atafanya ziara maeneo hayo.
"Komredi Makalla maelekezo yako ni amri kwangu. Nitakwenda Longido na Karatu. Tunashughulikia kero ya maji, tulifanya tathmini ya awali katika mji wa Karatu na kubaini kuna visima vilipata hitilafu. Ninamwelekeza Katibu Mkuu ndani ya wiki moja, tutaleta Sh. milioni 100 kurekebisha ili huduma irejee,” aliahidi.
Aweso alisema kuna mradi mkubwa wa zaidi ya Sh. bilioni nne unatekelezwa wilayani humo na kuwataka viongozi kusimamia vyem, ili kila shilingi iingie katika kutekeleza mradi huo na kuondoa tatizo la maji.
Alisema katika eneo la Longido, tayari mradi wa kutoa maji Mto Simba umeshakamilika na hatua inayofuata ni kuyasambaza katika Mji wa Longido.
Aweso aliwataka wananchi hao kuendelea kuiamini CCM kwa kuwa kwenye Ilani yake kuna utatuzi wa kero za wananchi.
Kero nyingine iliyoibuka ni kukatikatika kwa umeme ambayo Makalla alipotembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Longido Samia, aliona taa za sola ni nyinyi na alipouliza aliambiwa kuna tatizo la umeme.
“Wakati ninatembelea majengo ya shule hii, nimeona taa za sola nyingi, nimeelezwa kuna tatizo la umeme. Tunawaagiza TANESCO walishighulikie,” alisema Makalla.
Akiwa Longido Mundarara, alielezwa tena tatizo hilo ambako kote alimwita Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Arusha, Adelhem Mkulu, ambaye alisema njia ya umeme imelemewa kwa kuwa inahudumia umbali wa kilomita 1,000, hivyo kujengwa kituo cha kupooza umeme eneo la Karatu ili kuwezesha umeme kuwafikia bila tatizo.
Kero nyingine ni wananchi waliopisha upanuzi wa uwanja wa ndege Manyara unaotarajiwa kuanza Septemba, mwaka huu, kutolipwa mapunjo ya fidia iliyochelewa.
Mwakilishi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Arusha, alisema tayari wameshaandikia na mchakato unaendelea Wizara ya Fedha. Alisema fedha zilizolipwa ndio stahiki ya wananchi na hakuna aliyepunjwa kutokana na mtathmini wa serikali kupitisha na kuridhia.
Alisema kwa yeyote ambaye hakuridhika basi anapaswa kumwona Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya tathmini.
Kero nyingine ni barabara kati ya Longido na Mundarara, Kigongo hadi Sale inayokwenda wilaya ya Ngorongoro, ambayo imeharibika na kuwafanya wananchi washindwe kusafiri kuzifikia huduma muhimu.
Pia wilayani Karatu nako walieleza kuwa kero kubwa ni barabara nyingi kuharibika na kuomba kujengwa za kiwango cha lami, ambapo Mwakilishi wa TANROADS alisema kuwa serikali imetenga fedha za ukarabati na ujenzi wa barabara kuhakikisha zinapitika ikiwamo kujenga madaraja.
Kuhusu kero iliyoibuliwa kuwa wazee kutozwa fedha wanapokwenda kupata matibabu licha ya Sera ya serikali kuelekeza kundi hilo matibabu ni bure.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, alithibitisha kwamba walipokea malalamiko ya wazee hao na kwamba wengi huhitaji huduma za kibingwa ambazo hazipo katika ngazi ya wilaya, jambo ambalo linakuwa ni changamoto kuwahudumia.
Kero nyingine zilizoibuliwa zinahusu migogoro ya ardhi, ukosefu wa ajira, ndoa za utotoni ,kuziba kwa mifereji ya maji, mume kutelekeza familia baada ya kuuza mali, aliyenunua kiwanja kunyimwa njia na aliyemuuzia, wastaafu kupunjwa fedha zao, kutolipwa mishahara ya miezi mitatu na mwajiri.
Katika wilaya zote alizopita, Makalla aliwaelekeza wakuu wa wilaya husika kuandika mukhtasari wa kero zote na majibu yaliyotolewa, yakiwa nan amba za simu za walalamikaji kisha zifikishwe kwake kwa ajili ya ufuatiliaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED