Waziri wa Madini, Anthony Mavunde aeleza kuwa Serikali imeanza kutekeleza mradi wa kusaidia wachimbaji wanawake na vijana (Mining For A Brighter Tomorrow-MBT) kwa lengo la kuwainua kiuchumi.
Aliyasema hayo jana katika Kijiji cha Nyamishiga, Halmashauri ya Msalala aliposhiriki hafla ya utoaji wa leseni za uchimbaji mdogo 4 kwa kikundi cha wakina Mama cha TAWOMA Mshikamano.
"Mh. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anayo dhamira ya kweli ya kuwawezesha na kuwainua wachimbaji wadogo hususan wanawake na vijana. Na ndiyo maana amenipa maelekezo mahsusi ya kuwahudumia, kuwawezesha na kuwaendeleza wachimbaji wadogo, Rais ni mdau namba moja wa wachimbaji wadogo nchini.
Tutaendelea kutoa Leseni kwa wachimbaji wadogo nchini na kuwapanga vizuri ili kuchochea ukuaji wa sekta ya Madini.
Niwapongeze kikundi cha Mshikamano kwa kurudisha kwa Jamii(CSR) kupitia ujenzi wa Zahanati,Manunuzi ya gari la Wagonjwa na ujenzi wa nyumba za watumishi wa Afya,matumaini yangu ni kwamba mtafanya vizuri zaidi baada ya kuwakabidhi Leseni hizi.
Tunaendelea kushughulikia suala la upatikanaji wa nishati ya umeme ya uhakika na uboreshwaji wa miundombinu ya Barabara katika eneo hili,Aidha niendelee kukumbusha juu ya upunguzwaji wa tozo nyingi za Halmashauri kwa wachimbaji wadogo kama ambavyo iliridhiwa katika mkutano uliopita ulioshirikisha viongozi wa Halmashauri” alisema Mavunde
Akitoa salamu kwa niaba ya wanakikundi cha Mshikamano, Mama Semeni John Malale, Mwenyekiti wa TAWOMA Taifa alimshukuru Rais kwa namna anavyoendelea kuwajali wachimbaji wadogo hususan wanawake na vijana na kuahidi kwamba wanaenda kufanya shughuli za uchimbaji kwa kufuata taratibu zote na kulipa maduhuli ya Serikali kama inavyotakiwa ili kuchangia mapato.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Msalala, Idd Kassim alielezwa kufurahishwa na namna Serikali inavyoshughulikia changamoto za uchimbaji na kuiomba Serikali kuweka mkazo katika kuharakisha kufanya utafiti wa madini ili wachimbaji wawe na taarifa sahihi yalipo madini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kahama,Mboni Mhita alionesha wazi furaha yake na kumshukuru Dk. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyowaendeleza na kuwainua wachimbaji wanawake na vijana kiuchumi, na kuahidi kuwa ataendelea kuwapa ushirikiano wachimbaji wote ili wafanye shughuli zao kwa ufanisi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED