Waonywa kutanguliza fedha katika utoaji huduma za afya

By Beatrice Shayo , Nipashe Jumapili
Published at 11:46 AM Jun 30 2024
Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu.
Picha: Maktaba
Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu.

MGANGA Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu, ameagiza watoaji huduma nchini kuzingatia kuokoa maisha ya wananchi wanapofika katika vituo vya afya badala ya kuweka fedha mbele.

Prof. Tumaini ametoa agizo hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mahema ya wagonjwa waliokuwa wanapatiwa matibabu katika kambi maalum ya matibabu bure jijini hapa.

"Nitoe rai kwa watumishi wa sekta ya afya tutathmini uhai, hilo ndilo jukumu letu tulilopewa katika dhamana ya kutoa huduma kama muuguzi, mfamasia, daktari. Viapo vinatutaka kutetea uhai, tusiweke mbele fedha," amesisitiza Prof. Tumaini.

Mganga Mkuu wa Serikali amesema watumishi wa kada hiyo wanapaswa kutetea uhai wa wananchi ndipo fedha ifuate na kusisitiza viapo vilivyotolewa kwa watu wote ambao wanatoa huduma katika sekta binafsi na ya umma vinaelekeza hivyo.

Kuhusu kambi hiyo, amesema serikali imeunga mkono jitihada hizo katika kutoa vifaa na dawa na tayari watu zaidi ya 200 wamefanyiwa kipimo cha x-ray na wagonjwa wengine wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali za serikali.

Amesema hadi waliopelekwa katika hospitali za serikali wamepatiwa msamaha wa matibabu ya zaidi ya Sh. milioni 28 na zaidi ya vipimo 700 kwa siku nne.

Prof. Tumaini amesema kupitia kambi hiyo wamejifunza kwamba wapo waliofika wakihitaji huduma na wengine wakitaka kupatiwa huduma za kibingwa.

"Hospitali zote za halmashauri unapata x-ray na huduma za dharura unazipata huko, tunaendelea kupambana kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi ngazi ya chini ili wasihangaike kwenda umbali mrefu kufuata huduma za afya.

"Wengi waliofika hapa wana changamoto ya kifedha, ukiwa na bima ya afya una uhakika wa kupata matibabu kokote. Bima ya afya ndio suluhu na serikali imejipanga kusaidia wale ambao ni maskini kupata bima ya afya ili kila mwananchi aweze kupata huduma za afya," amesema.

Mganga Mkuu wa Serikali amesema huduma za mkoba zinaendelea na madaktari bingwa wanatoa huduma katika ngazi ya msingi ili kuwezesha wananchi kuzipata.

Amekumbusha jamii kujenga utamaduni wa kuangalia afya zao mara kwa mara kwa kuwa kupitia kambi hiyo, waliobainika kuwa na shinikizo la damu ni wengi, huku wengi wao hawakuwa na taarifa.

Pia amesisitiza jamii kuzingatia mlo kamili wa vyakula na kufanya mazoezi mara kwa mara, ili kujiepusha na maradhi ambayo yanazuilika.

"Ninaomba Watanzania wasipende kutumia dawa ovyo hasa hizi za antibaiotiki mpaka utakapoandikiwa na daktari.

"Ukifanya kinyume utasababisha usugu wa vimelea vya dawa na hatutakuwa na dawa ya kutibia haya magonjwa," amesema Prof. Tumaini.