JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linawashikilia wahamiaji haramu 13 kutoka Ethiopia, huku 11 kati yao wakikutwa hoi kwa kukoswa chakula, hivyo kulazwa katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga.
Watu hao walitekelezwa kwenye pango katika kijiji cha Wishiteleja wilayani Kishapu mkoani hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, alisema wahamiaji hao waliwakamata Agosti 8, mwaka huu, majira ya saa 12:00 jioni baada ya kupewa taarifa na raia wema na kuwakuta wakiwa katika hali mbaya kutokana na kukosa chakula.
“Walikuwa wamejificha katika pango na tulikuta mikate ikiwa imeoza pamoja na maji, ikimaanisha kwamba walikuwa wakiishi kwa kunywa maji na kula mikate. Hali zao kiafya zilikuwa mbaya sana,” alisema Magomi.
Kamanda Magomi alisema wahamiaji hao 11 bado wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao kiafya zinaendelea kuimarika, huku wawili wakiwakabidhi idara ya uhamiaji kwa ajili ya taratibu zingine za kisheria.
Alisema jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi ili kubaini mtu ambaye amewaletea wahamiaji hao haramu na kwamba hawawezi kuingia nchini Tanzania bila kuwa na mwenyeji. Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za wahalifu na wahamiaji haramu.
Mmoja wa wahamiaji hao, Maratha Rapson, akizungumza akiwa hospitalini, alisema walikuwa wanatoka Ethiopia wakienda Afrika kusini kutafuta kazi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED