UWT, Wabunge kufanya tathmini sababu za kuongezeka ubakaji,ulawiti

By Augusta Njoji , Nipashe Jumapili
Published at 10:48 AM Sep 08 2024
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Mary Chatanda.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Mary Chatanda.

KUTOKANA na kuwapo na wimbi la matukio ya ukatili wa kijinsia, ubakaji na ulawiti, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Mary Chatanda ameitaka Kamati ya Haki na Sheria ya umoja huo, wadau na wabunge kufanya tathmini ya kina ili kujua sababu za kuongezeka vitendo hivyo licha ya kuwapo na adhabu kali.

Akizungumza jana jijini Dodoma baada ya kuzindua kamati hiyo sambamba na kampeni ya msaada wa kisheria chini ya UWT, Chatanda amesema  tathimini hiyo ilenge kuona vifungu vya sheria vinavyohusika na makosa ya ubakaji na ulawiti kama vinahitaji marekebisho ya sheria na kutoa mapendekezo kwa serikali.

"Inasikitishwa na matukio haya ikiwemo ya hivi karibuni ya mtoto wa miezi sita kulawitiwa na kubakwa na baba yake mzazi hapa Dodoma hali iliyopelekea kifo cha mtoto huyo na tukio la kubakwa na kuawa kwa mama na binti yake, UWT inalaani matukio hayavna kuiomba Serikali yetu kuendelea kutafuta mwarobaini wa matukio haya ya kusikitisha," amesema.

Naibu Waziri TAMISEMI, Zainab Katimba.

Alisema UWT imekuwa mstari wa mbele katika ajenda ya kuhimiza maadili katika jamii na kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake ambapo ni moja ya kipaumbele chake.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Naibu Waziri TAMISEMI, Zainab Katimba amesema imeanzishwa kampeni ya msaada wa kisheria itakayoanza kwenye mikoa 10 na kila jumamosi ya mwisho wa mwezi kwenye ofisi za UWT kutakuwa na watoa msaada kisheria.

Amesema wanawake, watoto na watu wenye mahitaji maalum ndio walengwa kwenye kampeni hiyo na wameandaa program maalum kufikia watoto shuleni ili kupata elimu ya kujilinda na ukatili.

1