MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh. trilioni 2.34 kwa mwezi Julai ikiwa ni zaidi ya lengo lililowekwa kwa asilimia 104.4 kulinganisha na lengo la Sh. trilioni 2.246.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya Habari, iliyotiwa saini na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 20.9 ikilinganishwa na Sh. trilioni 1.94 zilizokusanywa Julai, mwaka jana, kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Alisema ufanisi katika makusanyo na ukuaji wa makusanyo kwa Julai, mwaka huu, ni wa kiwango cha juu kufikiwa na TRA katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
Mwenda alisema ufanisi huo umechangiwa na kuboresha uhusiano kati ya mamlaka na walipakodi kwa njia za mawasiliano na majadiliano.
Pia alisema hatua hiyo ni kutokana na kuchukua hatua za haraka katika vihatarishi vya ulipaji kodi pamoja na vitendo vya ukwepaji wa kodi.
Mwenda pia alisema kuongezeka kwa usimamizi wa watumishi wa TRA na kuendelea kuwapatia mafunzo kwa vitendo watumishi wapya kwa lengo la kuongeza uadilifu na weledi katika utendaji wao wa kazi.
Alisema wameongeza usimamizi wa matumizi sahihi ya Mashine za Kieletroniki (EFD) na matumizi ya Stempu za Ushuru wa Bidhaa (ETS).
Ufanisi wa makusanyo uliofikiwa na TRA kwa mwezi Julai, alisema ni kiashiria chanya katika kuhakikisha lengo la makusanyo kwa mwaka huu wa fedha la Sh. trilioni 30.4 linafikiwa.
Katika kufanikisha jambo hilo, alisema menejimenti ya TRA imejipanga kutekeleza mambo 12 ikiwamo maagizo yote yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuhusu usimamizi wa kodi.
Mwenda alisema hali hiyo pia imetokana na kuimarisha uhusiano na ushirikiano na walipakodi pamoja na wananchi wote, kuimarisha utoaji wa elimu ya kodi na huduma bora kwa walipakodi na kujenga na kuimarisha mifumo ya kodi za ndani na forodha.
“Kusimamia na kuimarisha misingi ya mfumo mzuri wa kodi ikiwamo haki na usawa katika utozaji kodi (No Favouritism or Victimization),” alisema.
Mwenda alisema mamlaka itaimarisha na kusimamia weledi taaluma yao na huduma nzuri kwa walipakodi ikiwamo watumishi wao wote kuvaa vitambulisho wanapotoa huduma ili kuweka uwazi baina ya mtoa na mpokea huduma.
Aidha, alisema watasikiliza na kutatua changamoto za kikodi za walipakodi kwa wakati nchi nzima.
“Kushirikiana na Tume ya Rais ya Tathimini ya Mfumo wa Kikodi Nchi ni ili kuwa na mfumo rafiki unaosimamia usawa, unaorahisisha shughuli za kiuchumi na wenye tija nchini,” alisema.
Mwenda alisema watasimamia utekelezaji wa makubaliano ya serikali na wafanyabiashara ikiwamo uwapo wa kodi elekezi kwa bidhaa nane zinazoingizwa nchini, na mfumo sahihi kwa biashara za kuchangia makasha (Consolidation).
“Kusimamia uadilifu kwa watumishi wa TRA na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria kwa wachache wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma,” alisema.
Alisema watakabiliana na vitendo vya ukwepaji wa kodi wa kukusudia, kwa kuimarisha upatikanaji wa taarifa hizo na kuendelea kujenga uwezo na uadilifu kwa watumishi, hususani katika ukaguzi na uchunguzi wa kodi za ndani na kimataifa.
Mwenda alisema wataendelea kurahisisha shughuli za kiuchumi nchini na kuongeza ulipaji wa kodi wa hiari.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED