Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha miradi mitatu ya ujenzi wa barabara zenye jumla ya Kilomita 111.4 mkoani Mara.
Miradi hiyo ni Ujenzi kwa kiwango cha lami Barabara ya Nyamuswa - Bunda-Bulamba(Km 56.4), Makutano juu - Sanzante (km 50) pamoja na barabara ya Musoma - Busekela(Km 92), kipande cha kwanza cha kutoka Kusenyi - Suguti (km5).
Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe amesema hayo tarehe 13 Machi 2024 alipozungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya ujenzi.
“ tunaishukuru Serikali yetu chini ya Mama yetu, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutoa kiasi cha shilingi Bilioni 137.165 ili kutekeleza mradi wa barabara hizi tatu ambazo ujenzi wake umekwishakamilika” amesema Mha. Maribe
Amesema kufunguliwa kwa barabara hizo kumeongeza uchumi wa Mkoa kwa kurahisisha usafiri kwa watalii wanaokuja nchini kuelekea Katika mbuga ya Serengeti; pia zimechochea fursa kwa wafanyabishara wa madini kuweza kuuza madini yao katika soko la kimataifa pamoja na kurahisha huduma ya usafiri wa kutoka Mkoa Mara kwenda Mikoa Jirani kwa uharaka zaidi tofauti na hapo awali.
Ametaja Miradi mingine inayoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami ni Barabara ya Sanzante- Nata ( Km 40), Mogabiri-Nyamongo ( Km 25), Tarime-Mugumu-(Km 87.14) sehemu ya Tarime-Mogabiri ( Km 9.3), Nyamongo-Mugumu (Km 48.15, na barabara ya Mzunguko ya Mugimu ( km 3.6), Ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha ndege Musoma, pamoja na Ujenzi wa Mzani wa kupima magari yakiwa kwenye mwendo.
Pia, ameishukuru Serikali kwa kuwajali Wakandarasi Wazawa kwani Miradi yote ya
Matengenezo ya barabara imefanywa na wakandarasi hao ikiwa ni juhudi za Serikali kuwajengea uwezo.
Mha. Maribe amesema taa zaidi ya 608 za barabarani zimefungwa katika maeneo ya Musoma mjini, Bweri, Nyabange, Butiama, Kiabakari, Sabasaba, Pida, utegi, mika, Mazami, Makutano (ziroziro) pamoja na Nyanchabakenye na mwaka huu wa fedha taa nyingine zaidi ya 336 zitaendelea kufungwa kwenye maeneo ya Kusenyi, Musoma Manispaa, Nyamuswa, Komaswa, Bitaraguru, Nyamika na Olio.
Ametoa wito kwa wananchi kuwa walinzi wa Miundombinu ya barabara ikiwemo taa na alama za barabarani na kuheshimu hifadhi ya barabara kwa kutofanya shughuli zozote kwenye maeneo hayo kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED