RAIS Samia Suluhu Hassan ameeleza kukerwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika kujinufaisha na kuagiza vyama vya ushirika na ugani kutathmini matatizo yaliyoko na kuyapatia ufumbuzi kabla hajaondoka madarakani.
Samia alisema hayo jana Ikulu ya Chamwino, Dodoma, wakati akizungumza na maofisa ugani na maofisa ushirika kutoka halmashauri zote Tanzania Bara.
Alisema moja ya mambo ambayo yanamkera ni viongozi wa vyama vya ushirika kutumia vibaya nafasi zao kujinufaisha kupitia jasho la wakulima.
“Kazi ya ushirika ni kusimamia haki za wanaushirika, lakini imekuwa sivyo viongozi wengi wanatumia nafasi zao kujinufaisha wao binafsi, badala ya wakulima walitumia nguvu zao kulima mazao yao,” alisema.
Rais Samia alisema vitendo hivyo vinavyofanywa na viongozi wa ushirika nchini ni dhambi kubwa.
“Leo mkulima kalima na kavuna lakini kiongozi ndiye anakuwa mnufaika wa mazao yale ambayo mkulima ametoa jasho lake. Ni dhambi kubwa sana. Kazi ya ushirika inapaswa kuwa ni kulinda maslahi ya wakulima, badala ya kuwa viongozi ndiyo wa kwanza kuminya haki za wanaushirika wao," alisema.
Kutokana na hali hiyo, Rais Samia alisema anataka kuona hali hiyo inabadilika ili ushirika uwe mtetezi wa wakulima, badala ya viongozi kuutumia kujinufaisha binafsi.
“Ninaomba matatizo yenu yote ambayo yamekuwapo mjitathmini na tuone nini cha kufanya ili kuyamaliza kabla muda wangu wa kuelekea Kizimkazi mwaka 2029,"alisema.
Rais Samia aliiagiza Wizara ya Kilimo kuhakikisha inatekeleza maagizo yake ya kuanzishwa kwa wakala wa huduma za ugani nchini.
“Wakala huu utumike kusimamia huduma za ugani nchini, lakini pia kutumika kwa ajili ya kuwapima wagani kwa huduma wanazo zitoa kwa wakulima,"alisema.
Alisema wakala huo pia lazima uwe na jukumu la kuwapima maofisa ugani kwa kazi wanazozifanya kuwasaidia wakulima nchini.
Rais Samia aliahidi kutoa Sh. bilioni tano kwa ajili ya kuchangia kuanzishwa kwa Benki ya Taifa ya Ushirika itakayosaidia kuimarisha vyama ushirika nchini na kuongeza tija kwa wanachama wake.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alisema serikali imeendeleza jitihada zake za kuwezesha sekta hiyo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Alisema jitihada hizo ni pamoja na kurudisha chanjo ya mifugo ya taifa ya mifugo ambayo iliondolewa kwa muda mrefu nchini.
“Ndani ya utawala wako, Mheshimiwa Rais umefanya mambo mengi sana katika sekta ya mifugo na uvuvi ikiwamo katika mwaka huu wa fedha, umetenga kiasi cha Sh. bilioni 28, kwa ajili ya kurejesha chanjo ya mifugo ya taifa, ambayo itasaidia wafugaji kuchanja mifugo yao,"alisema.
Ulega alisema serikali pia, imetoa mafunzo rejea ya teknolojia na maarifa mbalimbali kwa maofisa ugani 3,600 ambapo kati yao 3,100 ni wa mifugo na 500 wa uvuvi.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema serikali imewekeza fedha nyingi katika kilimo katika kipindi hiki cha miaka mitatu zikitumika pia katika ununuzi wa vifaa kwa ajili ya maofisa kilimo.
Pia alisema katika fedha hizo serikali imenunua magari , vifaa vya kisasa vya kupima udongo pamoja na pikipiki ambazo zimefungwa kifaa maalum cha kutambua ziliko.
Bashe aliagiza wakurugenzi wote wa halmashauri nchini kutenga bajeti kwa ajili ya kuhudumia shughuli za ugani ili kuongeza tija katika kilimo.
Vilevile aliwataka maofisa ugani wote nchini kutimiza majukumu yao ya kusaidia wakulima katika changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Mwakilishi wa maofisa ugani nchini, Enock Ndunguru, alisema kada hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo uhaba wa watumishi.
Alisema maofisa ugani walioko nchini ni 6,800, lakini mahitaji ni 20,000, hivyo kuchangia kushindwa kufika katika maeneo yote hasa vijijini kwenye uhitaji mkubwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED