Othman ahimiza matumizi fursa uchumi duniani

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 09:29 AM Aug 11 2024
Othman ahimiza matumizi fursa uchumi duniani.
Picha: Mtandao
Othman ahimiza matumizi fursa uchumi duniani.

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema kuna umuhimu kwa Tanzania kuweka mkazo wa kutumia ipasavyo fursa za kiuchumi zilizoko katika nchi za Afrika Mashariki na mashirika mbalimbali ya kimataifa ili kusaidia nchi kukuza Uchumi.

Othman aliyasema hayo juzi ofisini kwake, Migombani, mjini Zanzibar,  alipokutana na ujumbe wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulioongozwa na Waziri, Balozi Mammoud Thibiti Kombo. Ujumbe huo ulifika ofisini kwa Othman kujitambulisha kutokana na mabadiliko ya hivi karibuni yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Alisema kwa Tanzania, Afrika Mashariki si suala la uhusiano wa kijumuiya pekee bali ni fursa kubwa kiuchumi katika kuzitumia nchi za Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Uganda na zingine katika shughuli mbalimbali za kibiashara na kiuchumi, mambo ambayo alisema  zaidi ya ushirikiano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Makamu wa Rais alisema haja kubwa ya kujengwa uwelewa kwa wafanyabiashara na taasisi za serikali za  Muungano na Zanzibar katika kuainisha na kuzitumia fursa za kiuchumi zilizoko katika maeneo hayo jambo litakalochangia kwenda sambamba na kasi ya kiuchumi duniani.

Alisema hatua hiyo ni pamoja na kuwawezesha wananchi kwa kuwajengea uwezo wa kuzitambua na kuzitumia fursa hizo ili kuwa na tija katika kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa wananchi wa pande mbili za Muungano.

Pia alisema hatua hiyo itasaidia Watanzania kumudu kwenda sambamba na kasi ya maendeleo hasa  katika ulimwengu huu ambao kasi ya maendeleo ni kubwa sana.

Alizitaja baadhi ya taasisi za kimataifa kama vile Shirika la Haki Miliki (WIPO) lenye fursa kubwa za kiuchumi na kimaendeleo lakini  Tanzania na Afrika kwa jumla inakosa uwakilishi, hivyo kupoteza fursa nyinngi ambazo ni muhimu katika kuchangia uchumi na maendeleo.

Othman alisema kuna haja kwa wizara hiyo kuhasmasisha makongamano ya kibishara na ushirikiano yatakayowezesha Zanzibar kutumiwa vyema fursa za kipekee zilizopo ambazo zinaweza kuinufaisha nchi kiuchumi.

Naye Waziri Kombo alisema watajitihadi kuyatumia maelekezo waliyopata kwa viongozi mbalimbali ambayo yatawasaidia katika kuelata tija kwa matumizi ya fursa zilizopo.

Alisema  vita vya uchumi  duniani vinashinda vya silaha na kwamba kuna haja ya kufanya kila aina ya jitihada za pamoja katika kuhakikisha taifa linasonga mbele.