RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amesema kama Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepata kiburi baada ya kuona morali ya askari wake katika zoezi la Medani za Kivita la miaka 60 ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lililofanyika Pongwe, Msata, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Alisema tangu shamrashamra hizo zimeanza analishukuru jeshi hilo kwa kuendeleza ushirikiano na pia kuimarisha ushirikiano ya Jeshi la Ukombozi la China kwa kuwa ni sehemu ya kuwaenzi waasisi wa uhusiano huo.
Alisema mazoezi yote yaliyofanywa na JWTZ kueleza kuadhimisha miaka 60 ya jeshi hilo, kwa kushirikiana na Jeshi la China, Tanzania imepata fursa nzuri ya kubadilishana uzoefu wa kupambana na matishio mbalimbali ikiwamo ugaidi, uharamia baharini, usafirishaji binadamu na dawa za kulevya.
“Nimeshuhudia morali, nidhamu na utii wa makamanda wetu, nimepata kiburi najivunia jeshi letu, hatuna wazo la kumvamia mtu lakini si vyema kulegeza mkanda na muda wote tulitayarishe jeshi letu.
“ kupitia mazoezi hayo tumepata uzoefu mkubwa na kuimarisha ushirikiano wetu na watu wa China nakushukuru sana Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali John Mkunda.
“Nimefurahia shambulio la mchana, nimeona mpangilio wote wa makamanda wanavyopambana… nimefurahi sana”alisema Rais Samia wakati akifunga mazoezi hayo jana.
Aidha Rais Samia alichukua fursa hiyo kuwapongeza makamanda wanawake walioshiriki zoezi hilo kuwahimiza kuongeza juhudi katika kazi.
Alisema changamoto za jeshi hilo anazifahamu Serikali yake inazifanyia kazi.
Kwa upande wa CDF Mkunda alisema zoezi la Medani ya Kivita la miaka 60 ya JWTZ anamshukuru Rais kwa kuliwezesha jeshi kifedha na zana za kazi ikiwa ni sehemu ya kuliboresha jeshi lake.
Alisema lengo kubwa la zoezi hilo ni kuvipima vikosi vya utawala kuhudumia majeshi yao yanapokuwa porini badala ya kukaa maofisini.
“Tunakushukuru Rais kwa kuliwezesha jeshi lako kufanya zoezi hili kwa siku 14 lililowajengea utimamu, utii, morali na uaminifu askari na maofisa wetu ikiwamo kuwafunza kupigana na mtu binafsi, vikundi na kuwaweka vyema kisaikolojia”alisema CDF Mkunda.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED