Mwabukusi atema cheche baada ya kula kiapo

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 09:20 AM Aug 04 2024
RAIS mpya wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi
Picha: Mtandao
RAIS mpya wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi

RAIS mpya wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, amesema TLS ina jukumu la kuhakikisha amri za mahakama zinaheshimiwa ili kutotengeneza kizazi kama GEN-Z kilichoko nchini Kenya.

Mwabukusi aliyasema hayo jana baada ya kuapishwa katika mkutano mkuu uliofanyika jana jijini Dodoma, siku moja baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo. 

Juzi, mawakili walipiga kura kuchagua Rais mpya na nafasi zingine ndani ya chama hicho na matokeo ya uchaguzi kutangazwa usiku. Hata hivyo, mmoja wa wagombea katika nafasi ya urais, Sweetbert Nkuba, ametangaza kwenda mahakamani kuyapinga kwa madai kuwa kulikuwa na ukiukwaji katika kutangaza matokeo.

Mwabukusi alisema kama amri ambazo zimekuwa zikitolewa na mahakama nchini zitaendelea kutoheshimiwa, basi kuna hatari ya taifa kujenga kizazi ambacho kitakuwa na vurugu na maandamano kama ilivyo Kenya.

“Tukiendelea kukaa kimya vitendo hivi vya watu kupuuza amri za mahakama, wananchi watakosa imani na chombo hiki na kujenga kizazi cha GEN -Z ya Tanzania kama ilivyo sasa kwa majirani zetu Kenya.

“TLS tunalo jukumu kubwa sana kuona amri za mahakama zinaheshimiwa kwani mahakama ni chombo kinacho stahili kuheshimiwa sana, vinginevyo watu wataanza kutembea na mapanga.

“Kwa hiyo ni wajibu wetu kama mawakili kuhahakikisha amri za mahakama zinaheshimiwa, kuna sehemu mahakama ilitoa amri mtu atolewe, lakini hakutolewa sasa hali hii siyo nzuri kabisa kwa taifa,” alisema.

Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani, Mwabukusi alisema TLS ina wajibu wa kuhakikisha sheria na kanuni zinazingatiwa ili uwe  huru na haki.

“Ni kazi ya TLS ili kupata viongozi wenye sifa na uchaguzi kuwa huru na haki na kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza katika uchaguzi mara kwa mara nchini,” alisema.

Kadhalika, alisema TLS inahitaji kuishirikisha serikali kutambua haki za wananchi wake hasa katika masuala ya umiliki wa ardhi.

“Lazima TLS tuishirikishe serikali kutambua pia, wananchi wanahaki kama inahitaji kuwahamisha eneo fulani, lazima ijue kuwa wao pia, wanayohaki yao ya kumiliki maeneo hayo yenye historia ya maisha yao,” alisema.

MAKUNDI YAVUNJWE

Kuhusu uchaguzi wa TLS, Mwabugusi aliwaeleza wanachama kuwa kampeni zimekwisha na kutaka makundi kuvunjwa ili TLS kirudi kuwa moja.

“Uchaguzi umepita ndugu zangu. makundi yote yanapaswa kuvunjwa ili tuwe na TLS moja. Usiamini uko sahihi aliyekukataa anahaki kikatiba kwa hiyo tusitishe makundi yetu sote,” aliagiza.

Aidha, alisema katika uongozi wake TLS kitaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu walizojiwekea na si kwa msimamo wa mtu mmoja.

HOJA ZA NKUBA

Baada ya matokeo ya uchaguzi huo kutangazwa, Nkuba alisema hakubaliani nayo na tayari amewaagiza wanasheria wake kwenda mahakamani kupinga.

Mgombea huyo alidai kuwa anaamini kwamba uchaguzi huo umechakachuliwa kwa sababu pamoja na kamati ya uchaguzi kufahamu idadi ya wapigakura, haikupeleka karatasi za kutosha za kupigia kura, hivyo kulazimika kwenda kuchapisha zingine wakati uchaguzi ukiendelea.

Sababu nyingine, Nkuba aliitaja kuwa ni makubaliano yao yalikuwa mawakala kutoingia na vifaa vya mawasiliano katika chumba cha kuhesabia kura.

“Lakini katika hali ya kushangaza na kustaajabisha matokeo ya uchaguzi yalianza kutumwa mitandaoni na watu kuanza kumpongeza mtu aliyesadikika kuwa ndiye ameshinda,” alisema.

Mgombea huyo alidai kwamba hizo ni hujuma za kamati ya uchaguzi au kamati imeshirikiana na watu kuwapenyezea matokeo yasiyo rasmi na kuyatangaza nje na baadaye watu hao kufanya vurugu za kwenda kushinikiza kamati kutangaza matokeo wanayoyataka wao.

Nkuba alidai kuwa kamati ya uchaguzi au kwa kushirikiana na baadhi ya watu walishirikiana kuhujumu uchaguzi huo.

“Kwa hiyo ninaamini kamati imekosa weledi, msimamo na imehusika katika kuhujumu au kunajisi mchakato mzima wa uchaguzi kwa kutangaza matokeo ambayo hayaakisi uhalisia wa wapigakura na ubora wa kampeni na ubora wa mchakato ulivyokwenda.

“Kwa taarifa hii, ninaomba kuujulisha umma kwamba, ninakwenda mahakamani kupinga mchakato huu wa uchaguzi na kupinga matokeo na kubatilisha ushindi uliotangazwa na kamati ya uchaguzi.

“Naamini mahakama itasimamia haki na kuufuta uchaguzi huu ili kuitisha uchaguzi mpya kwa ajili ya kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa viwango na kwa kuzingatia weledi na usawa wa pande zote,” alisema.

UCHAGUZI ULIVYOKUWA

Uchaguzi huo ulianza saa 12:30 asubuhi juzi katika Ukumbi wa Mikutano Jakaya Kikwete, Dodoma, ambako vituo kadhaa vya kupigia kura viliwekwa na mawakili walijitokeza kutimiza haki yao ya msingi, huku askari polisi wakisimamia usalama.

Mchakato huo ulitarajiwa kufungwa saa 6.00 mchana, lakini kabla ya muda huo, karatasi za kupigia kura zilikwisha na kusimama kusubiri nyingine na matokeo kutangazwa usiku.

Wagombea wengine waliokuwa wakiwania urais ndani ya chama hicho ni Emmanuel Muga, Paul Kaunda, Revocatus Kuuli na Kapteni Ibrahim Bendera.

MAWAKILI WAPONGEZA

Mmoja wa mawakili, Dawson Chacha, ambaye alishiriki mkutano huo, alisema  walifurahishwa na matokeo hayo kwamba wamepata kiongozi waliokuwa wakimtaka muda mrefu.

Wakili Chacha alisema; “Kiongozi huyu ataongoza TLS kwa kipindi cha miaka mitatu tofauti na ilivyokuwa hapo awali, hivyo tunatarajia mambo makubwa hasa katika haki za mawakili, haki za wananchi, kwani kumekuwa na vitendo vya ukiukwaji wa haki kama vile ambavyo mmeona watu kutekwa na kupotea.”

Imeandaliwa na Paul Mabeja (Dodoma), Romana Mallya na Elizabert Zaya (Dar)