Mjumbe NEC: Kuna kundi linaichafua CCM

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 10:27 AM Jun 30 2024
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Rukwa, Sultan Saleh Seif.
Picha: Maktaba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Rukwa, Sultan Saleh Seif.

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Rukwa, Sultan Saleh Seif, ametoa ufafanuzi kuhusu hoja ya kuruhusu wananchi kuvua katika Ziwa Tanganyika ambao serikali imesitisha shughuli za uvuvi kwa miezi mitatu.

Amesema kuna kundi linatumia jina lake kutaka kuichafua CCM kisiasa na hata kumgombanisha yeye binafsi na uongozi wa chama hicho.

Seif ametoa ufafanuzi huo alipozungumza na Nipashe Jumapili baada ya kuwapo kipande kifupi cha video kinachosambazwa mitandaoni, kikimnukuu akiruhusu wananchi kuvua katika ziwa hilo.

Serikali imeshatangaza kufunga shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika kuanzia Mei 15 hadi Agosti 15 mwaka huu.

Seif amesema kuwa kipande cha video kinachosambazwa mitandaoni ni sehemu ya video ndefu iliyorekodiwa Juni 26 mwaka huu wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ninde, Kata ya Ninde, wilayani Nkasi wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara.

Hata hivyo, Seif amesema kipande hicho kimekatwa kwa ustadi kuonesha anapingana na serikali, akisisitiza hawezi kufanya hivyo, ana njia nyingi za kuikosoa na kuishauri serikali na si katika muktadha wa aina hiyo.

"Ukweli ni kwamba nilikuwa katika mikutano ya kawaida ya chama. Nilipofika katika kijiji hicho (Ninde), kukawa na malalamiko ya wananchi kuhusu kuzuiwa kuvua Ziwa Tanganyika.

"Nikampigia mbunge wetu, nikamweleza 'nipo Kijiji cha Ninde kwenye jimbo lako, nilipofika hapa nimewaeleza wananchi waliokusanyika kwamba unahitaji kuwasalimia na umewakumbuka sana… na leo huwezi kulala kama hujawasalimu'.

"Mbunge alisema (kama ilivyo katika video nzima ya mkutano huo) 'nipo bungeni ninaendelea kupambana kwa ajili ya Ninde, ninajua ilivyokuwa hapo kipindi cha uchaguzi mlikuwa hamna barabara, usalama wa Ziwa Tanganyika tunajenga kambi ya jeshi Kata ya Kizumbi, boti zitakuja kwa ajili ya patroo, wavuvi wanatakiwa wavue kwa usalama bila kubugudhiwa na majambazi.

"Pili, uvuvi wa mabwawani samaki kwaajili ya mboga unaruhusiwa (yowe likatawala) msizuiliwe kuvua samaki kwa ajili ya mboga, rukhsa hiyo ni kwa uvuvi wa ndoani, si kwa wale wanaotumia wavu, uvuvi wa ndoano mtu na familia yake kwenda kuvua pembezoni akale chakula kwa ajili ya mboga ni rukhsa."

Seif anaendelea kueleza kuwa, "Nilimpomwuliza mbunge kwamba baada ya mkutano huo wananchi waende wakavue samaki kwa kutumia ndoano, alijibu 'ndio'."

Kuhusu barua kutoka wizarani ya katazo hilo la uvuvi, mbunge alisema anashughulikia barua ya wizara kuja katika wilaya.

Baada ya maelezo hayo ya mbunge, Seif anasema aliwageukia wananchi, akisema (kama ilivyo katika video nzima) "muwe waadilifu, msiende huko mkavua kwa vitu ambavyo haviruhusiwi na hapa mmemsikia mbunge mwenyewe kasema na amezungumza na waziri, anayetakiwa kutoa rukhsa hii ni mkuu wa wilaya, hapa hayupo anayemwakilisha atamwambia haya ni maelekezo ya chama kwa kuwa hili jambo lipo kisheria."

Hata hivyo, Seif amesema kauli yake hiyo inapotoshwa makusudi kwa lengo la kumwonesha anapingana na maelekezo ya serikali.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, akitangaza uamuzi wa serikali kufunga kwa muda shughuli za uvuvi, amesema lengo ni kupumzisha shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu ili kuwezesha samaki kuzaliana na kuongeza tija kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao ziwani huko.

Ulega amesema uamuzi wa Tanzania unatokana makubaliano yaliyoazimiwa katika kikao kilichofanyika mwaka 2022, kikihusisha nchi zinazozunguka ziwa hilo ambazo ni Zambia, Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Ulega amesema uamuzi huo ni utekelezaji Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika unaoweka hatua na taratibu za usimamizi endelevu wa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.

Waziri huyo ameongeza kuwa uamuzi huo unatokana na utafiti uliobainisha kuwa kuna upungufu mkubwa wa samaki na dagaa katika Ziwa Tanganyika kutokana na ongezeko kubwa la uvuvi usio endelevu uliosababisha uharibifu wa mazalia ya samaki.