KUKIWA na hoja kwamba Rais aunde tume kuchunguza matukio ya utekaji watu nchini, miili ya watu watatu walioripotiwa kutekwa au kutoweka kwa nyakati tofauti, imepatikana.
Baadhi ya miili hiyo imekutwa ikiwa imenyofolewa viungo, huku watuhumiwa wakidai kutenda uhalifu huo kwa lengo la kupata utajiri.
Miili ya watu hao watatu imeripotiwa kukutwa katika mikoa mitatu tofauti. Watu hao wanadaiwa kuuawa katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Singida ndani ya mwezi huu.
Kati ya miili hiyo, upo uliokutwa umefukiwa ndani ya chumba chini ya kitanda na mwingine wa anayedaiwa Katibu wa Wazazi Tawi la Maguruwe, Kata ya Tandika, Temeke, uliokutwa umetenganishwa viungo na kufungwa katika viroba.
Mwingine umekutwa umenyofolewa sehemu ya siri kwa madai kuwa wahusika waliagizwa na mganga wa kienyeji kufanya hivyo ili kutajirika.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime, aliyasema hayo jana alipozungumzia matukio ya watu kutekwa na kutoweka katika mazingira yenye utata na baadaye kukutwa wameuawa.
"Tukio la kwanza ni la kijana Samwaja Saidi (22), mkazi wa Kijiji cha Chalunyangu, mkoani Singida. Alitoweka tangu Agosti 8 mwaka huu, katika mazingira ya kutatanisha na Agosti 23 mwaka huu, mwili wake ulikutwa umefukiwa katika shimo na sehemu za siri zikiwa zimekatwa," alisema.
Naibu Kamishna Misime alisema tukio hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi Makuro na kufunguliwa jalada la uchunguzi ambao ulianza mara moja.
Alisema katika ufuatiliaji wao, walipata taarifa kutoka kwa kijana mmoja ambaye alieleza kuwa siku ya tukio walikwenda na Said kutazama mpira na wakati wakirejea nyumbani walikutana na vijana wawili.
"Hao vijana wawili wakamwambia Saidi waende kunywa pombe. Tangu hapo hakuonekana tena na ndipo ndugu walipotoa taarifa polisi.
"Baada ya vijana hao wawili kukamatwa, walikiri siku hiyo walikwenda kunywa pombe na Saidi na wakati wanarejea nyumbani, walimnyonga na kumkata sehemu za siri na kufukia mwili katika shimo.
"Sababu za kufanya hivyo walieleza kwamba, walielezwa na mganga wa kienyeji wakiweza kupata sehemu za siri watakuwa matajiri," alisema.
Naibu Kamishna Misime alisema vijana hao walisema wako tayari kutoa ushirikiano walikofukia mwili huo.
Alisema kuwa baada ya taratibu kufuatwa, Agosti 24 mwaka huu, vijana hao walikwenda kuonesha eneo uliko mwili huo na ulitambuliwa kuwa ni wa Saidi.
"Hata hivyo, baada ya wananchi kushuhudia mwili huo, walikwenda nyumbani kwa mganga wa kienyeji kwa nia ya kuchoma nyumba yake moto, lakini Jeshi la Polisi lilituliza tukio hilo," alisema.
Naibu Kamishna Misime alitaja majina ya watuhumiwa hao ambao wanashikiliwa ni Seleman Nyandalu, maarufu Hango (24), mkazi Kijiji cha Chalunyangu, Saidi Msanghaa, maarufu Mangu (24), mkazi Kijiji cha Migungu na Kamba Kasubi (34), mganga wa kienyeji, mkazi wa Kijiji cha Migungu, Mtinko.
Katika tukio lingine, Naibu Kamishna Misime alisema lilitokea Dar es Salaam Agosti 19 mwaka huu; mwanamke Ezelia Kamana (36), mkazi wa Tandika Maghorofani, kudaiwa kuwa ametoweka au ametekwa.
"Jeshi la Polisi lilifungua jalada na katika uchunguzi ilibainika alikuwa na rafiki yake wa kiume, Abdallah Miraji, maarufu Musa (42), mkazi Sinza kwa Remmy, wilayani Kinondoni, ambao walikuwa na mgogoro.
Naibu Kamishna Misime alisema mwanamume huyo alikamatwa na alipohojiwa alikataa kufahamu aliko rafiki yake huyo.
Hata hivyo, Agosti 22 mwaka huu, walipokea taarifa katika Kituo cha Polisi eneo la Silversand, barabara ya Mtaa wa Freedom, Kunduchi kuwa kumeonekana mifuko ambayo ina viungo ambavyo vinadhaniwa ni vya binadamu.
"Polisi walifika eneo la tukio na kukuta mifuko minne ya viroba na katika kuichunguza, walikuta viungo ambavyo ni paja moja, vipande viwili vya mikono, eneo la kifua, makalio, 'matumbo' na nguo.
"Baada ya kupata viungo hivyo na mtuhumiwa kuelezwa, aliamua kueleza ukweli kwamba alimuua mpenzi wake na kutenganisha mwili wake katika vipande na kwenda kuvitupa maeneo tofauti," alisema.
Kamanda Misime alisema kuwa Agosti 23 mwaka huu, mtuhumiwa huyo aliongoza askari hadi eneo la Tegeta Block D na kuonesha alikotupa miguu na baadaye kuonesha alikotupa kichwa.
Katika tukio la tatu, Kamanda Misime alisema lilitokea jijini Tanga ambako mtoto Elia Elifaza (3), mkazi wa Kitongoji cha Kwedijava, wilayani Hendeni, alitoweka katika mazingira yasiyoeleweka nje ya nyumba yao tangu Agosti 19 mwaka huu.
Alisema taarifa ilitolewa polisi na uchunguzi kuanza na kukamatwa mtuhumiwa Jackson Elisante, maarufu Maeda (23), mkazi Kwedijava, eneo ambako kuna uchimbaji dhahabu.
Alisema kuwa baada ya kukamatwa na kuhojiwa, kijana huyo alikiri kumchukua mtoto huyo na kumkabidhi kwa mama yake mkubwa ambaye alikwenda naye wilayani Babati, mkoani Manyara.
"Askari waliambatana naye hadi Babati, lakini (mtuhumiwa) alibadili kauli na kueleza mtoto yupo kwa Kwedijava, wilayani Handeni, amemfukia ndani ya chumba amoishi.
"Walirejea Handeni na kuwaonesha chini ya kitanda katika chumba anamoishi alikomfukia mtoto huyo baada ya kumuua," alisema.
Naibu Kamishna Misime alitaja majina ya watuhumiwa wengine wanaoshikiliwa kutokana na tukio hilo kwa ajili ya uchunguzi ni Sadiki Lugendo, Mahiza Gumbo, Mwaligo Juma, Ali Mashaka, Juma Bakari, Abdulraman Suleiman na Bahati Daudi.
Alisema Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa watu kuacha tabia hizo zinazotokea ndani ya jamii na kusababisha wananchi kupotea au kutekwa na matukio kuhusishwa na wivu wa mapenzi, imani za kishirikiana, tamaa za fedha au kulipiza kisasi.
Kamanda Misime alisema Jeshi la Polisi pia linatoa angalizo kwa wanaozungumzia matukio hayo, watumie majukwaa yao kwa uangalifu, kwa kuwa sababu wanazozitoa ni kutaka kubadilisha ukweli wa yanayoendelea ndani ya jamii ili kuleta taharuki na kujenga uhasama.
"Tunatoa rai kwa viongozi wa dini, wazee wa kimila wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuona matatizo haya yanayotokea ndani ya jamii, hivyo waendelee kujenga misingi bora ya kuyazuia kuanzia ngazi ya familia.
"Jeshi la Polisi lingependa kutoa onyo kali kwa baadhi ya wananachi ambao wamekuwa na tabia ya kujichukulia sheria mkononi badala ya kufuata taratibu zilizoko za kuwasilisha malalamiko ili kupata ufumbuzi kwa mujibu wa sheria.
"Wakumbuke malalamiko au kero hata siku moja hazitatuliwi kwa njia ya kujichukulia sheria mkononi, kwani kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria ambapo husababisha madhara kwa maisha ya watu na mali zao," alisema.
Naibu Kamishna Misime alitolea mfano tukio la baadhi ya watu kujichukulia sheria mkononi ambalo lililotokea Agosti 22 mwaka huu, huko Lamadi, mkoani Simiyu la kwenda kuvamia Kituo cha Polisi na kuharibu mali.
Aliwataka wananchi wakumbuke kitendo cha aina hiyo ni kosa la jinai na kinasababisha madhara kwa binadamu, ambapo katika tukio hilo mmoja alifariki dunia, pia walizuia shughuli nyingine kuendelea.
"Tunatoa onyo wenye tabia kama hizo na yeyote mwenye mawazo ya kufanya uhalifu kama huu, Jeshi la Polisi lipo imara.
"Jeshi litachukua hatua kwa nguvu ileile ambayo watu wa aina hiyo wanatumia kutekeleza uhalifu wa kujichukulia sheria mkononi," alionya.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED