WAKATI vyama vya upinzani vikilalama kukatwa kwa wagombea wake, vimesimamisha wagombea 30,977 pekee kati ya nafasi 80,430 zinazowaniwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, aliyasema hayo jana jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema idadi hiyo ni sawa na asilimia 38.51 au theluthi moja ya nafasi zinazowaniwa katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu,
Mchengerwa alisisitiza kuwa takwimu hizo ni kabla ya kukamilika kwa hatua ya rufani za uteuzi, na zilizo sahihi za walioteuliwa zitatolewa baadaye.
“Katika nafasi zinazogombewa, vyama 18 vya siasa vimeweka wagombea katika nafasi 30,977 kati ya nafasi 80,430 sawa na asilimia 38.51, ukiacha Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimeweka wagombea katika nafasi zote, katika maeneo ambayo kuna mgombea wa chama kimoja atapigiwa kura ya ‘Ndiyo’ au ‘Hapana’, alisema.
Alisema katika nafasi za mwenyekiti wa kijiji zinazogombewa ni 12,280, vyama 18 vya siasa viliweka wagombea katika nafasi 6,060, sawa na asilimia 49.35 ya nafasi hizo.
“Nafasi za mwenyekiti wa mtaa zinazogombewa ni 4,264 ambapo vyama 18 vya siasa viliweza kuweka wagombea katika nafasi 3,281 sawa na asilimia 76.94 ya nafasi hizo.
“Nafasi za mwenyekiti wa kitongoji zinazogombewa ni 63,886 ambapo vyama 18 vya siasa viliweza kuweka wagombea katika nafasi 21,636, sawa na asilimia 33.87 ya nafasi hizo,” alisema.
Waziri Mchengerwa alisema hali hiyo ndio uhalisia wa uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali kwa vyama vyote vya siasa kabla ya malalamiko ya kuenguliwa kinyume na taratibu.
Alisema kutokana na Halmashauri za Wilaya za Kaliua, Nsimbo na Tanganyika kuwa na makazi ya wakimbizi ya Ulyankulu, Katumba na Mishamo na wananchi kuhama kwenye baadhi ya vitongoji kutokana na sababu mbalimbali, maeneo yatakayofanya uchaguzi Novemba 27, mwaka huu, kwa sasa ni vijiji 12,280, mitaa 4,264 na vitongoji 63,886.
RUFANI ZILIZOKUBALIWA
Alisema katika halmashauri zote kati ya rufani 16,309 zilizopokewa baada ya muda wa nyongeza wa siku mbili zilizokubaliwa ni 5,589.
Alisisitiza kuwa ilizingatiwa dosari ambazo zilisababisha kutoteuliwa kwao hazikuwa kubwa zinazoathiri matokeo yaliyokusudiwa na kanuni.
WAGOMBEA KUTOTEULIWA
Kuhusu dosari zilizosababisha baadhi ya wagombea kuenguliwa alizitaja kuwa ni kukosa sifa ya uraia wa Watanzania, kujidhamini wenyewe, kutojiandikisha kwenye daftari la wapigakura wa Serikali za Mitaa na wengine kuwa chini ya umri wa miaka 21.
Alisema wagombea wengi ambao hawakuteuliwa ni kwa mujibu wa vigezo vya kikanuni na kulikuwa na nafasi ya kuweka pingamizi dhidi ya mgombea au dhidi ya uamuzi wa Msimamizi Msaidizi na rufani endapo mlalamikaji asingeridhika na uamuzi wa Msimamizi Msaidizi dhidi ya pingamizi alilowasilisha.
UFAFANUZI WA TUHUMA
Alisema kuna viongozi vya vyama vya upinzani wametoa tuhuma ambazo baada ya ufuatiliaji waligundua hazikuwa na ukweli na zililenga kuleta taharuki na kuchafua mchakato wa uchaguzi uliokuwa unaendelea vizuri.
“Baada ya uteuzi wa wagombea Novemba 8, 2024, aliyekuwa Diwani wa Ubungo, Boniface Jacob alitoa tuhuma kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam wenye mitaa 636 wamekata majina ya wagombea wa CHADEMA 571 na yamebaki majina 45 tu na kuwa watendaji wa kata wamepewa maelekezo ya kutowateua wagombea wa CHADEMA, tuhuma hizi si za kweli,” alisema.
Alisema halmashauri za mkoa huo zina jumla ya mitaa 564 na sio 636 kama ilivyotajwa, ambapo katika mitaa hiyo CCM walichukua fomu mitaa yote 564 na CHADEMA walichukua fomu katika mitaa 437 kati ya mitaa 564 na waliteuliwa 282 na sio 45 kama ilivyosemwa.
“ACT walichukua fomu katika mitaa 219 na walioteuliwa 144, walioteuliwa na CUF walichukua fomu katika mitaa 148 na waliteuliwa 93.
“Kwa mara nyingine alieleza kuwa katika vijiji 32 vilivyopo katika Wilaya ya Rufiji wanachama wa CHADEMA wameondolewa wote, ni vyema umma ujue Wilaya ya Rufiji ina vijiji 38 na katika vijiji hivyo kuna vitongoji 178.
“Katika vijiji vyote 38 CHADEMA waligombea kijiji kimoja katika vitongoji 178, CHADEMA waliweka wagombea wawili sio kweli kusema kuwa katika Jimbo la Rufiji wagombea wote wa CHADEMA wameondolewa na ni vyema kuueleza umma kuwa hawakuweka wagombea katika maeneo wanayowataja,” alisema.
Kuhusu kufungwa ofisi siku ya kuwasilisha mapingamizi, Mchengerwa alisema ofisi yake ilifuatilia katika maeneo hayo na mengine nchini na kubainika kuwa hazikufungwa na wagombea walifanikiwa kupeleka pingamizi zao katika maeneo hayo.
Aliwasihi wadau wa uchaguzi huo kuacha kufanya propaganda ambazo hazina ukweli na zinazoleta taharuki inayohatarisha amani iliyopo.
Alisisitiza kuwa uchaguzi unazingatia Sheria na Kanuni za Uchaguzi na sio huruma ili kuhakikisha uchaguzi huo unaendelea kufanyika kwa misingi ya haki, usawa na utawala bora.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED