Kliniki ya Makonda yaongezwa muda

By Beatrice Shayo , Nipashe Jumapili
Published at 10:12 AM Jun 30 2024
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.
Picha: Maktaba
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

KUTOKANA na wingi wa wananchi kuendelea kujitokeza katika kambi ya matibabu mkoani Arusha, serikali imeongeza muda wa siku moja ili kila aliyejitokeza apatiwe huduma.

Vilevile, watu 700 waliobainika kuwa na shida kubwa kiafya, watatibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa gharama za serikali.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, alipozungumza na wananchi waliojitokeza kwenye kambi hiyo kupatiwa matibabu bila malipo iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

Amesema kinachofanyika katika kambi hiyo ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwa amezunguka nchini na kujifunza kwamba kuna Watanzania wengi ambao wanahitaji huduma za madaktari bingwa wabobezi lakini hawawezi kuzipata.

Naibu Waziri Mollel amesema kuna wengine wanakosa hata nauli ya kufika katika hizo hospitali kubwa.

"Wengine wanaweza kupata nauli lakini uwezo wa kujihudumia hawana, hivyo Rais alitoa maelekezo watoke na kushuka chini kuwafuata wananchi waliko," amesema.

Dk. Mollel amesema katika kambi hiyo wapo wananchi waliotokea katika mikoa mbalimbali, wamefika katika kambi hiyo ya matibabu ili kutibiwa.

"Wapo wananchi waliotoka mikoa ya Manyara, Singida, Dodoma, Kilimanjaro na wengine hadi wametokea Mbeya, maana yake pamefanyika hamasa nzuri ya kujua madakatri bingwa wabobezi wapo Arusha na hili tumpongeze Makonda," amesema.

Dk. Mollel amesema hiyo ni programu maalum ya kibingwa ya Rais Samia na tayari amesaidia kuwezesha kila huduma kupatikana bure kwa wananchi.

Amesema kuwa hadi juzi, jumla ya wananchi 28,976 wametibiwa na wale ambao wanatakiwa kwenda MNH ni 700 na watakaopelekwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wapo 200, watatibiwa kupitia programu hiyo ya Rais Samia.

"Kwa hapa Mkoa wa Arusha, kwa wale waliotoka wilayani walishindwa kwenda hospitali ya mkoa mpaka juzi waliotibiwa katika Hospitali ya Mount Meru ni 466. Maana yake mpaka Jumatatu tuliyoiongeza wananchi wengi watakuwa wamepata huduma," amesema.

Naibu Waziri amesema wananchi hao 28,976 ambao wametibiwa walishindwa kupata huduma kwa utaratibu wa kawaida, walihitaji kusaidiwa, hivyo wanahitaji kuongeza nguvu katika mkakati wa Rais Samia.

Amesema wanahitaji madaktari wao waendelee kushuka chini zaidi na kuongeza nguvu katika hospitali za wilaya kwa kuwa kuna wagonjwa wengi ambao hawakuhitaji hata kufika katika kambi hiyo, wangetibiwa hukohuko.

"Idadi ya watu inazidi kuongezeka, hawa wote walitakiwa kutoa fedha mfukoni wapate matibabu lakini hawana, wamekuja hapa.

"Katika hii huduma tumepata funzo kuwa inahitajika bima ya afya kwa wote, ni suala la kipaumbele," amesema Naibu Waziri Mollel.

Amesema anakwenda kuongeza idadi ya wafamasia wafike katika eneo hilo ili kupunguza foleni ya utoaji dawa kwa wananchi.

Amesema wataongeza pia madaktari ili kuhakikisha siku mbili zilizobaki wananchi wanapatiwa matibabu kwa wakati na kuondoa msongamano wa watu.

Makonda amesema wamesitisha kutoa namba mpya kwa wagonjwa kutokana na kuwapo idadi kubwa ya watu ambao hawajahudumiwa.

"Tunachoshindwa ni kuendelea kuongeza watu wakati tuliokuwa nao hatujawamaliza kuwahudumia tusingependa kuona hii hali inaendelea hadi Jumatatu, itakuwa haina faida walau tumalize tuliowapa namba ndio maana tumekubaliana kule tusitoe tena namba ili wote mhudumiwe waishe," amesema Makonda.

Makonda amesema tayari kuna wadau wengine jana waliwaletea dawa za Sh. milioni 31 kutoka Samiro Pharmacy Ltd na Benki ya NMB imewapatia dawa za Sh. milioni 10 na gari la kubeba wagonjwa.

Mkuu wa Mkoa huyo ameendelea kuomba wananchi kuzingatia utaratibu uliopangwa badala ya kuharibu foleni ili kila mmoja apatiwe matibabu.

WIZI WA SIMU

Wakati wananchi wakiwa kwenye foleni kwa ajili ya kusubiria matibabu, kuna tatizo limeripotiwa la kuibiwa simu zao, jambo lililozua taharuki.

Aliyekuwa akitangaza matangazo uwanjani hapo kila wakati alikuwa akipokea taarifa ya kuibiwa simu na kuwatangazia wananchi.

Ameeleza kuwa kuna wimbi kubwa la wizi wa simu unaoendelea kwenye foleni na wananchi kuombwa kuongeza umakini katika kulinda mali zao.

"Kuna wimbi kubwa la wizi wa simu unaoendelea, tunaomba muwe makini siyo wote wapo katika foleni ya ugonjwa,wengine ni wezi. Na wewe unayeiba simu tunakupa dakika 45 tutakukamata," ameonya.