Kanisa lamwalika Samia jubilee miaka 50

By Halfani Chusi , Nipashe Jumapili
Published at 09:19 AM Oct 20 2024
Picha ya kuunganisha ya Rais Samia Suuhu Hassan na Askofu wa AICT Dayosisi ya Pwani, Philipo Mafuja.
Picha: Mtandao
Picha ya kuunganisha ya Rais Samia Suuhu Hassan na Askofu wa AICT Dayosisi ya Pwani, Philipo Mafuja.

KANISA la Africa Inland Tanzania (AICT), Pastoreti ya Magomeni mkoani Dar es Salaam, limemwalika Rais Samia Suluhu Hassan katika jubilee ya miaka 50.

Sambamba na mwaliko huo, kanisa hilo limeahidi kutoa ushirikiano katika kuimarisha umoja, amani na utulivu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari, katika viwanja vya kanisa hilo jana, Askofu wa AICT Dayosisi ya Pwani, Philipo Mafuja, alisema lengo la mwaliko huo ni kuendesha harambee ya kukamilisha ujenzi wa kanisa  Sh. milioni 300.

"Tunatumia nafasi hii kuwaarifu mamilioni ya waumini wa kanisa la AICT kila mahali nchini kujumuika nasi iifikapo Oktoba 27, mwaka huu, hapa kanisani Magomeni.

“Ninaomba kutumia fursa hii pia kumkaribisha sana Mheshimiwa Rais Samia, ambaye ametupatia heshima kubwa kushiriki nasi siku hiyo pamoja na wengine wote watakaoambatana naye kuja kufanikisha harambee hii," alisema.

 Askofu Mafuja aliwashukuru Watanzania wa dini na madhehebu tofauti waliopokea kadi za michango ya sadaka ya ujenzi wa kanisa hilo, sambamba na  waliotoa ahadi ya kuchangia.

Alisema kuelekea siku hiyo, kutakuwapo na shughuli zingine za kijamii za kuonesha matendo ya huruma hasa kwa wale wenye uhitaji.

Pia alisema kanisa limepanga kugawa mitungi ya gesi kuunga mkono mpango wa serikali katika matumizi ya nishati safi ya kupikia na kutembelea vituo vya watoto yatima kuwajulia hali na kushirikiana nao.

Alisema miaka 50 ya kanisa imekuwa ya baraka kwa Watanzania kiroho na kimwili, kwa kuwa wameanzisha huduma katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwamo shule ambazo zimetoa mchango chanya katika maendeleo ya elimu.

Katika hatua nyingine, Askofu Mafuja aliwasihi wananchi kushiriki kujiandikisha na kupigakura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao, ili kuchagua viongozi wanaoona wanafaa kuwaongoza.