MAKAMU wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema changamoto kubwa zinazoisumbua Zanzibar ni kiwango kikubwa cha umaskini wa mahitaji muhimu pamoja na ukosefu wa ajira kwa vijana.
Hemed aliyasema hayo jana visiwani Zanzibar, wakati akifungua kongamano la kukusanya maoni ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Kutokana na changamoto hizo, Abdulla aliwataka wananchi kufikiri kwa kina namna ya kutatua changamoto mbalimbali za kijamii, pamoja na kutoa maoni yao kuhusu namna bora ya kuimarisha ustawi wa taifa.
“Tunapaswa kupanga na kuweka mikakati imara ya kuendelea katika matazamio ya muda mrefu kwa faida ya kizazi kijacho. Dira ya Maendeleo ya Taifa inayoandaliwa ni ya watanzania wote na si ya serikali ama ya chama fulani,” alisema Abdulla.
Alisema athari za mabadiliko ya tabia nchi, udumavu wa watoto kwa zaidi ya asilimia 30 na ukuaji mdogo wa matumizi ya teknolojia ni mojawapo ya masuala ambayo yamekuwa yakitatiza kasi ya maendeleo visiwani humo.
Abdulla aliomba wadau wa maendeleo, taasisi za umma na sekretarieti za mikoa, kuendelea kutoa maoni yao katika mchakato wa uandishi wa Dira Mpya, ili kuhakikisha inaakisi maoni ya wananchi.
Kwa upande wa timu ya kitaalam ya kukusanya maoni ya Dira Mpya, ilisema watanzania wengi wanataka serikali kujenga uchumi madhubuti, jumuishi, endelevu, shindani na stahimilivu katika jitihada za kupambana na umaskini.
Mhadhiri wa chuo kikuu Zanzibar na Mjumbe wa timu hiyo, Dk. Yahya Hamad Sheikh, alitaja maeneo mengine yaliyotajwa zaidi na wananchi, kuwa ni pamoja na maboresho katika huduma za kijamii, ikiwamo katika sekta ya afya, lishe, elimu, makazi bora na upatikanaji wa majisafi na salama.
Hamis Mnubi, mkazi wa Zanzibar, alishauri kuwa miaka 25 ijayo, kunatakiwa kuwa na uimara utawala bora, upatikanaji wa haki, ulinzi na usalama wa taifa pamoja na maendeleo ya sayansi, teknolojia na uvumbuzi kama sehemu ya kuharakisha maendeleo.
“Tunataka kuanzia sasa mpaka 2050, umeme usizimike tena Tanzania, kwa kuwa tumealika wawekezaji, tunajenga maghorofa yenye teknolojia ya umeme.
“Tuna treni ya kisasa SGR, hatutaki kusikia tena imekwama kwa sababu ya umeme,” alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED