Gambo amtuhumu Lema kuvuruga uandikishaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 08:27 AM Oct 20 2024
Gambo amtuhumu Lema kuvuruga uandikishaji
Picha:Mtandao
Gambo amtuhumu Lema kuvuruga uandikishaji

MBUNGE wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, amedai Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, amekodisha magari mawili aina ya Toyota Spacio na Toyota RAV 4, ili kufanya vurugu katika mchakato wa uandikishaji wa Daftari la Wakazi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Gambo alidai anaujua mpango wa Lema wa kukodi magari na kubeba wanafunzi kuwazungusha katika vituo vya uandikishaji, kwa ajili ya uchaguzi unaokuja.

“Ndugu yangu Lema mpango wake wa kukodi gari na kuwabeba wanafunzi kuwazungusha katika vituo vya kujiandikisha, kwa ajili ya uchaguzi ujao na wanafunzi ambao hawajatimiza umri wa kupiga kura, wakiwamo wenye umri wa miaka 15 hadi 18, tunaujua.

“Na video tunazo sema tu hatutaki kutoa, kwa sababu tutakosa kupata taarifa nyingine za mipango wanayoendelea nayo,” alisema.

Gambo alidai kuwa pamoja na Lema kupiga kampeni watu kujiandikisha, anashangazwa na kitendo chake cha kuonekana akijiandikisha juzi, jambo ambalo anasema sio sawa kwa kiongozi kusubiri nyakati za mwisho kwenda kujiandikisha.

“Tulitumia ushawishi mkubwa kumtaka Lema akajiandikishe, ilibidi nimtumie shangazi yangu (Mke wa Lema), ili amshawishi kwenda kujiandikisha na kwa kuwa ni watu wawili tu wenye kusikilizwa na Lema yaani Freeman Mbowe na Neema mke wake.

“Nimpongeze shangazi yangu kwa kufanikiwa kumshawishi hadi akaenda kujiandikisha na kuweza kutupia picha katika ukurasa wake wa Instagram,” alidai Gambo.

Alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejitosheleza, hivyo hakiwezi kufanya mambo yanayotuhumiwa na CHADEMA kuwa wanaandikisha wapigakura wasiokuwa na vigezo, ikiwamo kuwaandikisha wanafunzi ambao hawana umri unaohitajika.

Alisema walidai kuwa majina yanatumwa kwa njia ya mitandao ya kijamii, kwa ajili ya kuandikwa katika Daftari la Wakazi.

Nipashe ilipomtafuta Lema kwa njia ya simu kujibu tuhuma hizo, alisema hana cha kijibu na hawezi kuzungumzia jambo hilo.

Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alipopigiwa simu kujibu hoja hizo za Mbunge Gambo kutuhumu kuwapo kwa magari mawili yanayotumika kuleta vurugu katika mchakato huo, alikanusha madai hayo.

Alisema kama ni kweli Gambo ameona magari hayo, anatakiwa kuyakamata kuyapeleka Kituo cha Polisi, ili sheria ichukue mkondo wake.

“Kwa kifupi tu niseme, Gambo anatafuta kujibiwa na Lema, lakini hawezi kumzungumzia maana hana madhara yoyote kwake.

“Ameona Lema hamzungumzii popote, hivyo anaamua kutafuta aanze kumzungumzia na kuhusu hayo magari anayosema kama ana uhakika ameyaona ayakamate ayapeleke polisi, ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

“Kwa nini anazungumza na nyinyi waandishi wa habari na wakati Jeshi la Polisi lipo. Kwanini asiwaeleze,” alisema Golugwa.