Biteko ataka mikataba uchimbaji wa makaa ya mawe inufaishe taifa

By Elizabeth John , Nipashe Jumapili
Published at 09:40 AM Aug 04 2024
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka.
Picha: Mtandao
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka.

SERIKALI imesema haitakubali kuanza miradi mikubwa ya uchimbaji chuma na makaa ya mawe kabla ya kupata mikataba bora itakayonufaisha taifa.

Pia, imewatoa hofu wananchi mkoani hapa hususani Wilaya ya Ludewa kuwa madini ya makaa ya mawe na chuma yatachimbwa, lakini mikataba itakayoingiwa ni lazima iwe bora ikilenga kuwanufaisha.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, alitoa kauli hiyo juzi wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa uchimbaji wa madini ya chuma Maganga Matitu wilayani Ludewa, mkoani humo ulioingiwa kati ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na Kampuni ya Fujian Hexingwang Industry Tanzania Co. Ltd.

 Alisema serikali haiwezi kukubali wakati wowote kuona mgeni anafika nchini na kuchimba rasilimali halafu anaondoka huku akiwaacha wanashangaa na kuulizana kila mmoja kuwa imekuaje.

 “Hatutakubali kuona uongozi wa mgodi au kiwanda kitakachojengwa viongozi wote wanatoka nje ya nchini, kwani hata mkataba ulioingiwa wa uchimbaji wa madini ya chuma tumekubaliana baadhi ya nafasi kushikwa na Watanzania na nyingine wageni,” alisema Biteko.

 Alisema hayo yote yatawezekana iwapo nchi itakuwa na amani ambayo itasaidia kuvutia wawekezaji.

 Aliwataka wawekezaji waliopata nafasi ya kuwekeza nchini kuwa na uhakika na hawatopata hasara kwa sababu nchi ina mazingira mazuri ya kibiashara na mahali ambapo inaonekana kuna kasoro zinarekebishwa mara moja.

 Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, alisema mradi wa Maganga Matitu ulioko wilayani Ludewa una umuhimu mkubwa na kutegemewa katika kukuza uchumi wa nchi. 

“Utekelezaji wa mradi huu, kwanza unatarajia kuwezesha ukuaji wa uchumi na kuchangia katika mnyororo wa thamani katika nchi yetu na ni matarajio kwamba, uchumi wa viwanda sasa unakwenda kukua,” alisema Kigahe.

 Mkurugenzi Mtendaji wa NDC, Dk. Nicolous Shombe, alisema mradi huo wa uchimbaji wa madini ya chuma unaogharimu zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 77 ambazo ni mtaji kutoka kwa wawekezaji, ni wa kwanza hapa nchini ambao unakwenda kuchochea maendeleo ya viwanda.

“Tunatarajia mradi utachukua miaka mitatu kwa hiyo mwaka 2027 utaanza uzalishaji na wananchi wa pale ambao ni zaidi ya 300 wanakwenda kulipwa fidia ya Sh. bilioni 4.2 kabla ya mwezi Januari mwakani,” alisema Shombe.

 Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, alisema mkoa huo utaongoza kwa kuweka mazingira nafuu zaidi kwa kila atakayefika kwa ajili ya kuwekeza.

 Naye Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamonga, alisema kitendo cha kutiwa saini mkataba huo kitafungua ulipaji wa wananchi kwa wananchi waliopisha mradi huo.

 “Fidia za hawa ni chache tunaamini watalipwa mapema iwezekanavyo ili ujenzi uanze,” alisema.