WMA yapongeza wakulima Karatu kuzingatia matumizi sahihi vipimo

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 10:36 AM Aug 11 2024
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) Albogast Kajungu (kulia) akiongoza zoezi la kuhakiki uzito wa vitunguu vilivyofungashwa tayari kwa kuuzwa katika eneo la Mang’ola wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha, Agosti 9, 2024.
Picha: WAM
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) Albogast Kajungu (kulia) akiongoza zoezi la kuhakiki uzito wa vitunguu vilivyofungashwa tayari kwa kuuzwa katika eneo la Mang’ola wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha, Agosti 9, 2024.

KAIMU Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Albogast Kajungu, amefanya ziara ya kushtukiza katika mashamba ya vitunguu eneo la Mang’ola, Karatu mkoani Arusha na kuridhishwa na wakulima wanavyozingatia matumizi ya vipimo sahihi.

Akizungumza na timu ya wataalamu wa WMA juzi wakati wa ziara hiyo , Kajungu alisema lengo ni kujiridhisha ikiwa wananchi wanazingatia elimu inayotolewa na wakala kuhusu matumizi ya vipimo sahihi ili kulinda pande zote, yaani wakulima, wafanyabiashara na watumiaji wa bidhaa. 

Katika ziara hiyo, timu hiyo ya wataalamu wa WMA, walihakiki uzito wa vitunguu vilivyofungashwa katika vifungashio vya aina mbalimbali tayari kuuzwa pamoja na kuzungumza na wakulima, wafanyabiashara na wasafirishaji wa mazao hayo.

“Niwapongeze sana kwa kuzingatia matumizi ya vipimo sahihi maana katika mazao yote yaliyofungashwa ambayo tumepima, hakuna yaliyozidi uzito unaoelekezwa kisheria. Nawasihi mwendelee hivyo kwani kila upande utapata faida stahiki,” alisema Kajungu.

Kuhusu maelekezo ya kisheria kwa uzito wa mazao ya shamba yaliyofungashwa, Kajungu alisema mkulima yuko huru kufungasha kwa kutumia aina yoyote ya kifungashio isipokuwa azingatie uzito usizidi kilo 100.

Alitoa ufafanuzi huo kutokana na uelewa tofauti kwa baadhi ya watu wanaotafsiri kuwa sheria inakataza kufungasha mazao kwa kuongeza kishungi katika vifungashio.

“Niendelee kuwaelimisha na kuwaelewesha kuwa tafsiri sahihi ya lumbesa si kishungi bali ni uzito uliozidi kilo 100 kwa mazao yaliyofungashwa. Katika  hili niseme wazi huwezi kuthibitisha lumbesa kwa macho, hivyo ni lazima upime kujiridhisha kuwa mazao yaliyofungashwa yamezidi kilo 100,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, alishauri halmashauri zote nchini kutumia mizani kupima mazao yaliyofungashwa ili kuondoa utata na manung’uniko yanayojitokeza kwa baadhi ya wakulima na wafanyabiashara kwamba wanatozwa faini kwa mazao yaliyofungashwa na kuwa na kishungi yakitafsiriwa kama lumbesa.

“Mwarobaini wa changamoto hiyo ni kutumia mizani kama sheria inavyoelekeza na si kutizama kwa macho,” alisema. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima na wafanyabiashara wa vitunguu katika eneo la Mang’ola walikiri kunufaika zaidi kila upande baada ya kuanza kuzingatia elimu ya vipimo sahihi waliyopatiwa na serikali kupitia WMA. 

Marietha Tlemai, mmoja mkulima wa vitunguu, alipongeza serikali kupitia WMA kwa kuwajali wakulima na kuweka sheria ya ufungashaji mazao inayolenga kulinda maslahi yao.

Awali, timu hiyo ya wataalamu kutoka WMA, ilitembelea ofisi ya  mkuu wa wilaya ya Karatu ili kueleza dhamira ya ziara yao na kupokewa na Katibu Tawala, Dk. Lameck Karanga, ambaye aliwahakikishia kuwa ofisi yake inaunga mkono jitihada za kutokomeza lumbesa ili kulinda maslahi ya wananchi ambao wengi hujishughulisha na kilimo cha vitunguu.