NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo, amewataka wananchi ambao hawajapata vitambulisho vya uraia wakavichukue sehemu walikojisajili.
Sillo alitoa rai hiyo juzi jijini Dar es Salaam baada ya kufanya ziara katika sehemu zinazochakata vitambulisho hivyo.
Alisema kitendo cha serikali kutoa Sh bilioni 42.5 kwa ajili ya kuhakikisha waliopata namba wanapatiwa vitambulisho vya taifa kimeleta matokeo chanya.
"Vitambulisho 20,000,000 tayari vimeshasambazwa kwa wananchi, ambao bado hawajachukua watatumiwa meseji kwenye simu zao inayo waonesha mahali kwa kwenda kuchukua kitambulisho na kumaliza kilio chao.
"Nimegundua wapo wanaojisajili zaidi ya mara moja na kwa majina tofauti hali hiyo inawapa tabu wahakiki kwa kuwa vitambulisho hivyo ni kwa ajili ya usalama wa taifa" alionya Sillo huku akisifu utendaji kazi wa NIDA (Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa),” alisema.
Sillo alisema, tayari NIDA imeanza kuifanyia kazi changamoto hiyo kwakuwa hawawezi kutoa vitambulisho bila kujiridhisha au kuwa na taarifa sahihi.
Kadhalika, aliwataka baadhi ya wananchi kuepuka tabia ya kupeleka taarifa za uongo wanapohitaji vitambulisho akisisitiza kufanya hivyo hakutawasaidia.
Mkurugenzi James Kaji, James Kaji, alisema mtu anapofikisha umri wa miaka 18 atembelee kituo cha uandikishaji ili apate kitambulisho kwa sababu kumekuwa na mrundikano wa wahitaji pale nafasi za kazi zinapojitokeza au za chuo.
Alisema kwa sasa wameweka mfumo wa kuwatumia meseji ambapo wanatarajia mpaka mwishoni mwa mwezi huu vitambulisho vyote viwe vimechukuliwa.
Alisema tangu juzi walipoanza kutumia mfumo wa kutuma meseji tayari zaidi ya watu 400,000 siku hiyo kuanzia asubuhi mpaka mchana walipatiwa vitambulisho.
Alisema kutokana na mwitikio huo mpaka kufikia mwisho wa mwezi huu vitambulisho vyote vitakuwa vimechukuliwa.
"Ninapata kesi nyingi kuna walioachishwa kazi kama 600,000 hivi kwa majina feki sasa wanataka kurudi kwaajili ya kutumia majina yao halisi lakini wakiweka alama ya kidole jina linasoma lilelile wamekuwa wengi ni wapiga kelele ninaomba acheni kupiga kelele kwa kuwa hilo ni kosa kisheria kwa sababu walifoji," alisema Kaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED