Washauri klabu za fedha shuleni

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 10:08 AM Aug 11 2024
Washauri klabu za fedha shuleni.
Picha: Mtandao
Washauri klabu za fedha shuleni.

SERIKALI imeshauriwa kuwasimamia wakuu wa shule kuongeza kasi ya kuanzisha klabu za mambo mbalimbali yakiwamo ya fedha katika shule ili zitumike kutoa elimu hiyo na mambo mengine ya kijamii.

Ushauri huo ulitolewa juzi na Mlezi wa Klabu katika Shule ya Sekondari ya Kutwa Liwale, Mwalimu Mustafa Likambako, alipokutana na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha ambayo iko mkoani hapa kutoa elimu ya masuala ya fedha kwa makundi mbalimbali ya wananchi wakiwamo wanafunzi, wafanyabiashara, wakufunzi na wajasiriamali. 

“Katika shule yetu tuna klabu tatu za mazingira, masuala ya rushwa na femina. Kwa kuwa mimi ndiye mlezi wa klabu hizo, nimeona zinavyowasaidia wanafunzi kuwa na uelewa mpana wa masuala ya kijamii  wanayojifunza muda wa ziada,” alisema.  

Alisema kuna umuhimu kwa Wizara ya Fedha kuanzisha klabu ya masuala ya fedha katika shule mbalimbali ili wanafunzi wafundishwe matumizi ya fedha tangu wakiwa wadogo ili wakiwa wakubwa wawe na uelewa wa masuala hayo. 

“Shuleni kwetu tuna matamasha ambayo huwa tunatumia jukwaa hilo kuwashindanisha wanafunzi wa klabu mbalimbali na kutoa zawadi. Hii inasaidia kumfanya mwanafunzi awe makini darasani lakini kuwa na juhudi binafsi yakusoma na kushika wanachofundishwa”, alisema Likambako. 

Alisema iwapo zitaanzishwa klabu za masuala ya fedha katika shule itasaidia kupata mabalozi ambao ni wanafunzi na wakirudi nyumbani likizo wanakuwa walimu wazuri kwa wazazi na jamii inayowazunguka. 

Naye Ofisa Mchambuzi Hesabu Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Mariam Mtunguja, alisema wametoa elimu ya masuala ya fedha kwa makundi mbalimbali wakiwamo wanafunzi, wakufunzi, vikundi vya wajasiriamali na wafanyabiashara. 

“Tumeona kiu ya wanafunzi kuuliza maswali mengi wakitaka kujua mitaji inatakiwa kuanzia shilingi ngapi, lakini waliuliza kama wanafunzi wanaruhusiwa kuwa wawekezaji nimeona kuna umuhimu wa elimu hii kuanza kutolewa mapema katika shule mbalimbali”, alisema Mtunguja. 

Mwanafunzi  wa Shule ya Sekondari Liwale Day,  Zuleikha Hamidu, aliahidi kuanza kuweka akiba kwenye fedha za matumizi anazopewa na wazazi wake ili kumsaidia kwa baadaye.