WAKULIMA, wafugaji na wavuvi wa mikoa ya Kanda ya Mashariki ambayo ni Morogoro, Tanga, Dar es Salaam na Pwani, wameelezwa kuwa wana kila sababu ya kufanya vizuri kutokana na kubarikiwa kuwa na taasisi kubwa za sekta hizo katika mikoa yao.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batlida Buriani, alisema hayo juzi wakati akifungua Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi, maarufu Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, mkoani hapa.
Alisema katika sekta ya kilimo, mkoa wa Morogoro kuna Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na taasisi mbalimbali za utafiti wa kilimo na kwamba endapo wakulima watavitumia kikamilifu wataongeza uzalishaji na tija, hivyo kulingizia taifa mapato.
“Wenzetu wa SUA hapa Morogoro wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika sekta ya kilimo, hivyo wakulima wakija katika maonesho haya watafaidika na kila elimu wanayotaka kuhusu kilimo, hivyo hakuna sababu ya sisi Mikoa ya Kanda ya Mashariki kushindwa kufanya vizuri,” alisema.
Kuhusu mifugo, Balozi Dk. Buriani alisema kwenye mkoa wa Tanga kuna Taasisi ya Kitaifa ya Mifugo (TARIRI) ambayo wafugaji wa Kanda ya Mashariki wana uwezo wa kuitumia kwa ajili ya kuboresha mifugo yao ikiwamo kunenepesha na kufuga kisasa.
Akizungumzia uvuvi, alisema kwa Mkoa wa Dar es Salaam ipo Taaisisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) ambayo imekuwa ikitoa mchango mkubwa kuimarisha sekta hiyo, hivyo hakuna sababu ya kushindwa kufanya vizuri.
Mkuu huyo wa mkoa alisema asilimia 65 ya Watanzania kwa sasa wako kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ambazo wanachangia pato la Taifa asilimia 28 kutokana na bidhaa wanazozalisha na asilimia 24 kuuzwa nje ya nchi.
Kuhusu maonesho hayo, alisema kila mwaka yamekuwa yakiimarika kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wanaotembelea kwa ajili ya kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo, ufugaji na uvuvi.
Alisema mwaka 2023, watu 75,000 walitembelea maonesho hayo na mwaka huu wanategemea yatatembelewa na watu zaidi ya 80,000 huku idadi ya washiriki ikiongezeka kutoka 589 mwaka 2023 na kufikia 596 mwaka 2024.
Awali, akisoma taarifa ya Maonesho ya Kanda ya Mashariki kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele, alisema lengo ni kutoa elimu kuhusu masuala ya kilimo, ufugaji na uvuvi ili kujifunza mbinu mbalimbali za kuongeza tija.
Meja Gowele alisema kupitia elimu hiyo, makundi hayo matatu yatapata ufumbuzi wa changamoto zao sambamba na kuongeza tija, hivyo kutoa mchango mkubwa kwa taifa kupitia sekta hizo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED