Viongozi, vijana wasaka fursa kiuchumi

By Halfani Chusi , Nipashe Jumapili
Published at 09:53 AM Sep 01 2024
Uchumi
Picha: Mtandao
Uchumi

WADAU wakutana kuweka mikakati ya kutumia fursa za kiuchumi zilizoko jijini Dar es Salaam, ili kuwanufaisha vijana wanaokabiliwa na ukosefu wa ajira.

Walikutanika juzi mkoani hapo kupitia Jukwaa la Maonesho ya Vijana lilikuwa sehemu ya Mradi wa Youth Ready (YR), chini ya mpango wa miaka minne unaoongozwa na World Vision Tanzania na kuungwa mkono na Barrett Family Foundation ya Canada.

Mradi wa YR unalenga kuwawezesha vijana walio nje ya shule kuwa na afya njema, tija na mawakala wa mabadiliko wanaoshiriki kijamii.

Akifungua kongamano hilo lililokutanisha viongozi na vijana zaidi ya 200, Joseph Mhaiki, Mwakilishi kutoka World Vision Tanzania, alisema wamelenga kujadili uvumbuzi wa biashar.

Mhaiki alisema pia, wamelenga kujadili kusoma na kuandika kidijitali na uongozi wa kimataifa, kuhimiza vijana kuchangamkia fursa na kuleta mabadiliko chanya.

Alisema kwa ushirikiano kati ya Asasi ya Umoja wa Mataifa (UNA) Tanzania na Shirika la Afya na Maendeleo ya Wanawake (KIWOHEDE), wanasisitiza dhamira ya kuwawezesha vijana ili kuchochea maendeleo ya taifa.

Alisema katika mpango huo wa YR unaotekelezwa  katika Kata za Kivule na Kipunguni wilayani Ilala, Dar es Salaam, una lengo la kuwafikia vijana 1,400 kabla ya kujitanua katika maeneo mengine.

Alisema mpango huo utafanya kazi kwa karibu na washirika mbalimbali ili kuhakikisha kuwa unatekelezwa vyema na kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa kubadilisha fikra na maisha ya vijana.

Ibrahim Mwenda, Mkurugenzi Mtendaji wa UNA Tanzania, alisisitiza umuhimu wa kuongezeka kwa ushirikiano kwa ajili ya kuwawezesha vijana. 

“Jukwaa hili litasaidia kufungua mawazo ya vijana kwa fursa zinazopatikana kwao,” alisema Mwenda.

Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Shigeki Kombatsubara, aliwahimiza vijana kutumia zana za kidijitali kwa maendeleo yao.

Mnufaika wa Mpango wa Vijana Kiongozi, Monica John, alisema kuwa mafunzo aliyopata chini ya mpango huo, yamepanua uelewa wake na yametolewa wakati muafaka, ambapo vijana wengi wanakabiliana na changamoto za ajira.