Othman: Mabadiliko kidemokrasia, kiuchumi, kisiasa haki ya wananchi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 09:46 AM Sep 01 2024
MWENYEKITI wa Chama cha ACT - Wazalendo, Othman Masoud Othman.
Picha:Mtandao
MWENYEKITI wa Chama cha ACT - Wazalendo, Othman Masoud Othman.

MWENYEKITI wa Chama cha ACT - Wazalendo, Othman Masoud Othman, amewaeleza vijana kwamba mabadiliko ya kidemokkrasia, kiuchumi na kisiasa na kimaendeleo ndani ya taifa lolote ni haki ya wananchi.

Amesema wananchi ndio wapigakura ili kuamua kiongozi gani ashike madaraka ya uongozi katika nchi yao. 

Othman aliyasema hayo juzi katika ukumbi wa Five Star, Kiembe Samaki wilaya ya Magharib ‘B’ Unguja, alipokuwa akifungua  Kongamano la Vijana wa Mkoa wa Mgaharibi B Kichama lililojadili nafasi ya vijana katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Kutokana na hali hiyo, Othman aliwataka vijana  kufahamu kwamba wao ndio chachu ya mabadiliko hayo yanayohitajika sasa ndani ya Zanzibar katika kuhakikisha inakuwapo   Zanzibar mpya yenye uwezo na nafasi ya kupiga hatua zaidi kiuchumi na kimaendeleo kwa kutumia vyema rasilimali za nchi.

Alisema vijana hawana budi kufahamu kuwa hakuna nchi yoyote inayoweza kupiga hatua kiuchumi na kimaendeleo bila kuwa na mamlaka kamili ya kuzitumia ipasavyo rasilimali za ndani zilizoko katika kukuza ajira na maendeleo na kutumia soko la ndani lililopo kwa kuuza biashara ya bidhaa zitakazozalishwa.

Kwa mujibu wa Othman, kazi muhimu ya serikali ni kuwajengea uwezo wananchi hasa vijana  kuweza kupata ajira zenye staha na kupata kipato ili kupambana na umasikini jambo ambalo linahitajika sasa Zanzibar kama zilivyoweza kufanya nchi zingine  duniani na kupiga hatua kimaendeleo.

Pia aliwataka vijana kutambua kwamba Mapinduzi ya Zanzibar yalilenga kuleta mabadiliko ya kisiasa na kujenga uzalendo kama ilivyofanyika katika nchi mbalimbali duniani kwa vyama vya ukombozi lakini kutokana na kushindwa kutimiza matakwa ya wapigakura vyama hivyo  vimeondolewa madarakani na wananchi  na kuweka uongozi wanaoamini kwa matumaini ya kimaendeleo.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, aliwasisitiza  vijana hkuendelea kuandaa makongamano ya namna hiyo ili kuwaelimisha na kufahamu mustakabali  wa maendeleo yao na taifa kwa jumla.

Aliewahimiza vijana  kuachana na ndoto za kupata uongozi wa udiwani, uwakilishi au ubunge na badala yake fikra zao zilenge katika kuleta mabadiliko ya kweli kwa mustakabali wa taifa.

Naye Naibu Katibu Mkuu  wa ACT- Wazalendo  (Bara), Ester Thomas,  aliwataka vijana kutokubali kufanywa ngazi ya kupitisha na kuingiza watu kwenye madaraka ambao wataiangamiza nchi na kwamba vijana ndio ukombozi wa nchi.

Akifungua Kongamano hilo, Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Magharibi Kichama, Malik Juma Mohammed, aliwataka vijana kutobweteka na badala yake wahakikishe  wanakuwa na vitambulisho na kuandikishwa kuwa wapigakura kwa kuwa wao ndio wenye jukumu la kuleta mabadiliko ya  kidemokrsasia Zanzibar.