VAR ije kusaidia waamuzi, na kamwe isiongeze utata

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:35 AM Jun 15 2024
VAR
Picha: Mtandao
VAR

SASA ni rasmi Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza tangu historia yake, itakwenda kutumia mashine za mfumo wa video kusaidia marefa kufanya uamuzi sahihi uwanjani.

Hiyo ni baada ya serikali kupendekeza kutoa msamaha wa kodi katika uingizaji wa vifaa hivyo hapa nchini.

Katika Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2024/25, aliyoisoma juzi Bungeni, Dodoma, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu  Nchemba, akipendekeza hayo alisema, uwepo wa VAR utaondoa malalamiko ya maamuzi yasiyo sahihi, kwa waamuzi kutoona vyema kutokana na kasi ya mchezo au upendeleo.

"Msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara tutaanza kutumia VAR ili kuhakikisha matokeo yanayopatikana uwanjani yanakuwa ya haki, ili tuwe nazo za kutosha katika viwanja vyote, ninaleta pendekezo la kutoa msamaha katika  uingizaji mashine hizo na vifaa vyake kwa ufafanuzi utakaotolewa hapo baadaye, " alisema wakati akiwasilisha mapendekezo ya bajeti ya mwaka.

Tunaipongeza Serikali kwa kuwa sikivu, ambapo wamekuwa wakiyafanyia kazi haraka mambo mbalimbali ya kimichezo, na hata malalamiko ya mashabiki wa michezo nchini, hususan soka.

Kuwepo kwa VAR katika ligi yetu imekuwa ni kilio cha muda mrefu ili kupunguza malalamiko ya baadhi ya waamuzi, hasa ikihusu zinazoitwa 'timu kubwa' au 'timu pendwa'.

Tanzania itakuwa ni moja kati ya nchi chache sana Afrika kuwa na ligi ambayo itakuwa na usaidizi ya maamuzi ya kiteknolojia.

Hii inaonyesha vile vifaa vya VAR ambayo vinaletwa kwa msaada wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), itakayofungwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam haitatozwa kodi.

Miezi michache nyuma, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), Wallace Karia, alibainisha moja wa wadhamini wa Ligi Kuu Tanzania wataleta VAR inayotembea, ambayo kitaalamu inaitwa 'mobile VAR.'

Akasema hii itakuwa inasafiri mikoani kwa ajili ya kufanya kazi katika viwanja mbalimbali kama itakavyoelekezwa na Bodi ya Ligi.

Karia amependekeza iwe inakwenda katika michezo yenye mvuto, inatazamwa na watu wengi, na mashabiki wengi pia.

Kwa hili lililofanywa na serikali, mashine  hiyo nayo itaingizwa ikiwa ndani ya msamaha.

Nashauri pia taasisi zingine, wadau na wafanyabiashara, kuchangamkia fursa kwani wanaweza kununua na kuleta mashine hizo nchini, wakafanya biashara ya kuzikodisha ili zikafungwe katika viwanja mbalimbali.

Uhakika ni mpaka sasa ni VAR mbili tu, hivyo fursa imepatikana kwa watu kuleta zingine, hasa zile zinazotembea, ili mechi zote nane za Ligi Kuu ziwe na mashine hizo.

Hata hivyo, ushauri wangu ni kuwapo na mafunzo pia kwa waamuzi kwa ajili ya kutoa maamuzi sahihi, kwani uwepo wake pekee haisaidii.

Ninavyojua VAR haitoi maamuzi, ila inamsaidia kumwonyesha mwamuzi ili atoe maamuzi yaliyo sahihi, je tumewandaa marefa wetu kwa ajili ya kuitafsiri?

Tunaona katika baadhi ya Ligi za Ulaya, bado makosa ya waamuzi yanaonekana na wanalalamikia. Nadhani wakati VAR zitafanya kazi, kuwepo na mafunzo kwa waamuzi, pamoja na uadilifu kwa sababu wanaweza pia kutafsiri sivyo kwa matakwa yao, kama ilivyoonekana katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Tunataka VAR isaidie waamuzi pale ambapo hawajaona kwa sababu ya kasi ya mchezo, au wamepitiwa, warudie kufanya uamuzi sahihi na siyo ije kuleta utata mwingine wa waamuzi kuanzisha kigugumizi, na kuweka pembeni uamuzi sahihi licha ya mashine huyo kuonyesha wazi tukio.

Kama waamuzi hawatakuwa na mafunzo sahihi, ujasiri, uadilifu na upendeleo, itakuwa kazi bure. Kazi sasa kwa TFF na Bodi ya Ligi kufanya kila kinachowezekana kwa waamuzi, ili VAR iwe kweli mwarobaini wa maamuzi tata.