Ratiba ya Ligi Kuu itoke mapema timu zijipange

By Mhariri Mtendaji , Nipashe
Published at 10:53 AM Jun 24 2024
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi nchini (TPLB), Almasi Kasongo.
Picha: Maktaba
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi nchini (TPLB), Almasi Kasongo.

HIVI majuzi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi nchini (TPLB), Almasi Kasongo, alisema wameshaanza kutengeneza ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara ya msimu ujao.

Akaongeza kuwa msimu ujao wanatarajia kutengeneza ratiba bora zaidi ambayo itakuwa na uzani sawa kwa klabu zote na zitawapa muda makocha na wachezaji kujiandaa, kupata muda wa kufanya mazoezi na kusafiri kwenda vituoni kwa wakati.

Tunaipongeza Bodi ya Ligi kwa kuliangalia hilo, kwani msimu uliopita kulikuwa na baadhi ya timu zinacheza mechi mbili baada ya siku tatu, kitu ambacho ni hatari kwa afya ya wachezaji, lakini hushusha ushindani.

Tunatamani kuona angalau ratiba hiyo inatoa nafasi kwa timu kucheza mechi mbili kwa wiki ama moja, ili kutoa muda wa wachezaji kupumzika, na pia makocha kupata nafasi ya kuvitengeneza vikosi vyao na kuondoa mapungufu ambayo wameyaona.

Msimu uliopita baadhi ya makocha walikuwa wakilalamika kutokuwa na muda wa kurekebisha mapungufu kwa sababu ya kubanwa na ratiba, matokeo yake timu ikicheza mechi hii, inakwenda kucheza nyingine bila kufanya maandalizi yoyote kwa sababu muda mfupi wanaoupata wanautumia kwa safari.

Hata kama kila siku kuanzia Jumatatu hadi Jumapili kutakuwa na mechi ya Ligi Kuu, lakini TPLB inatakiwa kutazama timu itakayocheza siku husika kuipa angalau siku tatu kabla ya kucheza mechi nyingine.

Tukiachana na hilo ambalo Bodi wanasema watalifanyia kazi, kuna suala la kutangazwa kwa ratiba mpya.

Tumekuwa tukishuhudia wakati mwingine ratiba ikitangazwa wiki mbili tu kabla ya ligi kuanza. Hii si sahihi hata kidogo. Bodi ya Ligi ijitahidi ratiba ya msimu mpya itoke angau mwezi mmoja kabla ya kuanza na hilo linawezekana.

Tumeona tayari ratiba ya Ligi Kuu England itakayoanza Agosti 16, mwaka huu imetoka kabla hata ya Julai.

Ni kwamba siku ya ufunguzu, Machester United itacheza dhidi ya Fulham na Agosti 17, michezo sita itachezwa.

Yaani Chama cha Soka nchini humo kimetoa ratiba ya msimu mpya, kabla hata wachezaji hawajaanza maandalizi ya msimu mpya (pre season), kwani ndiyo kwanza wako mapumziko.

Hivyo makocha na wachezaji wataanza maandalizi wakiwa wanafahamu mechi ya kwanza watacheza na timu gani, na zinazofuata, hivyo kuwa na nafasi ya kujiandaa kutokana na aina ya mpinzani wanaokwenda kukutana nao.

Mfano, tayari Fulham wanafahamu watafungua na Manchester United, kwa hiyo wameshajua watakwenda kuwakabili vipi. Makocha kufahamu aina ya timu wanazokwenda kukutana nazo mapema kunawapa muda wa kutengeneza mifumo ya kukabiliana nao, kwani kila timu ina staili yake ya uchezaji.

Huku kwetu inawezekana mpaka timu zinaanza 'pre season' zitakuwa hazijui zitaanza na nani na wapi, hivyo tunaikumbusha TPLB kulimulika hilo kwa kuhakikisha ratiba hiyo inatoka mapema.

Ifike wakati bodi hiyo kubadilika na kuanza kutoa ratiba mapema, hata ili timu zipate kujiandaa vema jambo ambalo litaongeza ushindani katika ligi yetu.

Inawezekana kuwa hivyo kwa sababu Kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (CAF), imeshatoka, ambapo mechi za awali za Ligi ya Mabingwa na Shirikisho, zinaanza Agosti na Oktoba mpaka Desemba na hatua za makundi, mtoano hadi fainali itakuwa Machi hadi Mei mwakani.

Hivyo Nipashe tunashauri na ratiba ya Ligi Kuu kutoka mapema kwani itazipa nafasi timu kujiandaa na mpinzani wanaokwenda kukutana naye, kuandaa mipango ya usafiri pamoja na kufahamu aina ya viwanja ambavyo watakwenda kuvitumia.