Wanawake wasikwamishwe kugombea uongozi

Nipashe
Published at 11:25 AM Jun 25 2024
Wanawake wasikwamishwe kugombea uongozi.
Picha: Maktaba
Wanawake wasikwamishwe kugombea uongozi.

BAADHI ya wanawake hukatishwa tamaa kugombea nafasi za uongozi kisiasa kutokana na vikwazo wanavyokumbana navyo.

Wengine wanakosa ujasiri wa kuthubutu baada ya kuona wenzao wanavyopata misukosuko ikiwamo kudhalilishwa na kutukanwa kwenye majukwaa.

Hali hiyo inathibitishwa na baadhi ya viongozi wanawake waliowahi kushika nyadhifa za juu serikalini na kwenye taasisi mbalimbali, mikikimikiki waliyopambana nayo mpaka kufanikiwa kushika uongozi.

Miongoni mwa sababu zinazowadhoofisha wanawake wengi kujitokeza kuwania nafasi iwe kwenye siasa au taasisi ni kuombwa rushwa ya ngono.

Kuna wanawake wanaojitambua ambao wakishatajiwa suala la rushwa ya ngono, anaona isiwe tabu na kuamua kuendelea na mambo yake anayofanya kuliko kudhalilishwa.

Sehemu yoyote linapokuja suala la kupewa nafasi kwa upendeleo, ufanisi hukosekana kwasababu ya kukosekana kwa heshima.

Rushwa ya ngono ni kilio kikubwa sehemu za kazi na kwenye vyuo vya elimu ya juu.

Mtu hata kama ana haki ya kupandishiwa mshahara, au cheo anaweza kutafutiwa sababu ya kukwamishwa kwasababu tu hakutoa ushirikiano alipoombwa kutoa rushwa ya ngono.

Hii ni vita kubwa na inapaswa kukomeshwa na wanawake wenyewe kwa kujitambua na kutokubali kudhalilishwa kwa namna yoyote ile.

Kwenye nafasi za kisiasa, wanawake wengi hulalamika kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji kwa kuitwa majina ya ajabu ajabu ili tu wakatishwe tamaa.

Kwa wanawake walio kwenye ndoa wanakuwa kwenye mtihani mkubwa baada ya wenza wao kusikia yanayofanyika kwenye mchakato wa kuwania nafasi hizo na kuamua kuwakataza ili kuepuka kashfa.

Suala hili linahitaji kukemewa na pia elimu ya kutosha kuanzia mijini na vijijini ili wanawake wengi waelimike na kujitokeza kuwania nafasi.

Vyama vya siasa, wanaharakati wa haki za binadamu mna kazi kubwa ya kutoa elimu kupiga vita jambo hilo.

Kwa kudhoofisha wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi, kunaweza kukapoteza ari yao ya kuonyesha vipaji vyao vya uongozi.

Na katika maeneo mengi ya kazi imeshuhudiwa kuwa wanawake wanapopewa uongozi wanafanya vizuri na hata suala la rushwa ya ngono huwezi kulisikia.

Mapambano ya rushwa ya ngono ni lazima yawe makubwa ili kukomesha hali hiyo kabisa.

Aidha, wanawake wajitahidi kuhamasishana wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali wasibakie kuwa wapiga kura.

Katiba inaruhusu kugombea, kupiga kura na kupigiwa, lakini bado hawajitokeza kwa hofu ya udhalilishaji.

"Vikwazo vipo vingi vinavyowafanya wanawake washindwe kujitokeza kugombea, sababu moja wapo hatuna uthubutu, pili, elimu ya uraia haiwafikii kinamama nje ya miji, juhudi zifanyike wafikiwe. Rushwa ya ngono ni kikwazo, waume zetu wakisikia unataka kugombea wanakukataza kama haujaolewa wazazi wanakukataza kugombea," anasema aliyewahi kuwa waziri wa zamani Shamim Khan.

Mwanamke akitaka kugombea nafasi yoyote anapaswa kukataa rushwa ya ngono na akiwa na heshima yake hakuna atakayemfuata.

Pia ni muhimu wakajua kanuni na vyama vya siasa vifanye bidii kupeleka kanuni hizo hadi ngazi ya chini ndipo watapatikana wanawake wengi.

Kuna nafasi za viti maalum vya udiwani na ubunge, ambazo zimependekezwa na wadau wa siasa ziwe na ukomo wa miaka kumi ili kutoa nafasi kwa wanawake wengine kuziwania.