SAKATA la kupewa uraia kwa wachezaji wa Singida Black Stars, Emmanuel Kwame Keyekeh, Josephat Arthur Bada na Mohamed Damaro, ndiyo limekuwa gumzo wiki hii nchini.
Keyekeh raia wa Ghana, Bada wa Ivoct Coast na Damaro, akitokea Guinea, kwa sasa ni raia wa Tanzania baada ya wao wenyewe kuomba kwa mujibu wa Idara ya Uhamiaji.
Taarifa ilisema walipewa kwa mujibu wa vifungu vya 9, 23 vya Sheria ya Uhamiaji, sura ya 357, wakitajwa kuwa ni raia wa Tanzania kwa Tajnisi.
Kupewa uraia kwa wachezaji hao kumeibua hisia kutoka kwa wanamichezo, raia wa kawaida na wanasheria kila mmoja akiongea lake, lakini baadhi wakiamini hawakupaswa kupewa kutokana na kutokidhi vigezo vingi vilivyowekwa kwa uombaji.
Baadhi wakaenda mbali na kusema hata ule 'uspesho' wa wachezaji hao kwa ajili ya kuichezea timu ya taifa, hawauoni, kwani pamoja na kwamba ni wazuri, lakini si bora kiasi cha kulazimika kuwapa uraia kwa mtindo huo.
Pamoja na hayo, sheria za Shirikisho la Mpira wa Miguu (FIFA), ukizisoma haziwapi wachezaji hao nafasi ya kuichezea Timu ya Taifa, Taifa Stars.
Zinasema hivi. Mchezaji aliyebadili uraia anapaswa kuishi kwenye nchi yake mpya kwa miaka isiyopungua mitano ili apate sifa ya kuichezea timu ya taifa. Sidhani kama wanayo.
Mchezaji anapaswa kuwa amesafiri kwenye nchi yake hiyo mpya akiwa na umri wa miaka 10 na 18, huku FIFA wakihitaji ushahidi wa tiketi, visa, vibali vya ukazi vyenye na tarehe sahihi.
Tatu, FIFA watachunguza kama sababu ya kubadili uraia mchezaji haikuwa ya kimpira, yaani wakigundia alibadili ili acheze timu ya taifa, hawatoi ruhusa hiyo.
Kwa maana hiyo, wachezaji hao raia wa Tanzania wataendelea kuitumikia Singida Black Stars kwenye mechi zake za Ligi Kuu.
Inawezekana wachezaji wameomba ili kuipunguzia mzigo wa vibali vya kuishi na kufanya kazi katika klabu yao.
Au pia wameomba kwa kukubaliana na klabu kutokana na kuzidisha idadi ya wachezaji 12 wa kigeni iliyowekwa kikanuni. Kwa maana hiyo Singida itakuwa na wachezaji 12 wa kigeni, na hao watatu hivyo ingekuwa na wachezaji 15 ambao hawajazaliwa nchini.
Mimi nadhani imefika wakati Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), kuongeza wachezaji wa kigeni msimu ujao kutoka 12, angalau kuwa 15.
Nadhani wakati wa kutoa maoni ya idadi ya wachezaji wa kigeni, kamati zifikirie namna gani ya kuongeza zaidi kuliko kupunguza.
Wadau wengi wa soka nchini wanabainisha kuwa vipaji vya wachezaji nchini vimezidi kupungua, na hata wachezaji wa Kitanzania ambao wana vipaji, mara nyingi havina mwendelezo kutokana na mambo mbalimbali, ikiwamo nidhamu ya kuishi kwa wanamichezo, hivyo wengi hata timu zinazoitwa au kujiita ndogo, nazo zimeamua kusajili kutoka nje ya nchi.
Nafikiri kuongezwa kwa idadi ya wachezaji kutawafanya wachezaji wanaozaliwa Tanzania kuanza kujitafakari upya, kujitambua, kupigania namba, kujitunza, lakini pia kutazifanya mamlaka kutolazimika kutoka uraia kwa Tajnisi, kirahisi hivyo.
Nafikiri pia, hakuna wachezaji wengi wa nje watakaoomba, kwani nadhani ufinyu wa idadi ya wageni wanaoruhusiwa kwa klabu moja ndiyo sababu ya yote haya na si vinginevyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED