Msimu juisi, matunda sawa kiafya, ila yapo magonjwa ya uchafu

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 10:01 AM Nov 21 2024
Msimu juisi, matunda sawa kiafya, ila yapo magonjwa ya uchafu
Picha:Mtandao
Msimu juisi, matunda sawa kiafya, ila yapo magonjwa ya uchafu

KATIKA kanuni za kiafya, matunda tunatajiwa kuwa yamo katika orodha muhimu ya mlo, kwa manufaa yetu kiafya.

Hilo tunakubali tukiwa na walau ufahamu wa kihistoria, kwamba mtazamo mmojawapo ni kwamba tunapokula matunda, basi tujue tunalinda miili yetu. 

Tukirejea katika uhalisia wa kinachoendelea kimaisha ni kwamba, sasa inajulikana kwamba ni msimu wa matunda nchini na yanapatikana kila kona.  

Kuanzia sokoni na mtaani tunakopatikana, kuna aina ya mauzo kupitia nyenzo za baiskeli, pia magenge mitaani, sokoni ndiko usiseme inapatikana katika namna mbalimbali. 

Kama nilivyogusa awali, kwa nafsi yangu nipazungumzie zaidi Dar es Salaam, mahali niliko. 

Leo ni msimu wa matunda na wahitaji wako wanapatikana kwa wingi, Hapana shaka wajasiriamali nao wanatumia fursa zilivyo, kuwa wakala wa kuisambaza ziwafikie wahitaji kila waliko, kwao nao mbali na kuwa watoa huduma, wako ndani ya riziki ajira. 

Baadhi ya watu wameingia kufanya biashara ya kuuza matunda ya kukata matunda ya kuuza yakiwa mazima huku wengine wakifanya biashara ya juisi. Kila mhitaji kwa staili yake anapata chake. 

Hiyo yote ni moja ya watu kujiingizia kipato kupitia biashara hiyo. Lakini, tukisimamia ‘vigezo na masharti kuzingatiwa’ katika mahali hapo pa kujiingzia kipato, katika sura ya pili inatakiwa wafanyabiashara hao kukumbuka wakati wote usalama wa afya kwa watumiaji, iwe juisi au tunda. 

Nina eneo lialonigusa kwa upekee, wauza matunda ya kukatwa. Baadhi yako katika maeneo ambayo si rafiki kiafya, kwa ajili ya kufanyiwa biashara za namna hizo. 

Baadhi unakuta taka zimejazana, halafu pembeni mtu kaweka matunda yaliyokatwa kama vile tikiti, nanasi na maembe. 

Wapo wanaouza matunda yaliyokatwa na wanayahifadhi katika vifungashio na wapo wanaouza matunda yaliyokatwakatwa na kuyaweka mezani pasipo hifadhi yoyote ya kiafya. Hatari ndiyo inapoanzia hapo! 

Kwa kufanya hivyo wanaotumia vifungashio wanakuwa wamewalinda walaji, lakini kwawanaokata tunda na kuliweka wazi mezani lilivyo, ni wazi hawawalindi walaji tarajiwa. Maana uchafu unafika mahali hapo moja kwa moja. 

Kwa upande wao wauza juisi, tunaona wapo baadhi ya wafanyabiashara wanaojali afya za wanywaji juisi. 

Anagalizo hilo nalitoa, ilhali kwenye masoko ninawaona waliojiajiri wameweka mashine za kusaga juisi, mteja akinunua matunda sokoni na anahitaji kusagiwa anapata huduma hizo. 

Hiyo ni hata kabla ya kuchukua chake kama muuzaji au mlaji, anaanza safari yake kwenda kuzitembeza juisi kwa wafanyabiashara walengwa. 

Nitumie nafasi hii nihoji, kwa wanaosaga juisi sokoni kukoje, kuanzia juisi yenyewe, maji ya kusaga na usalama wake kwa ujumla ukoje? 

Maana tunajua juisi maandalizi yake maji ya yanatakiwa yawe safi na salama. Sasa hao walioko sokoni juisi wanazosaga maji yanayotumiwa. kweli yawe na si ya usalama. 

Nasema hivyo, maana katika umma tunajuana, kuna wasio na mashine za kusaga juisi, hivyo wanalazimika kusagia sokoni na kwenda nyumbani kujichanganyia maji. 

Pia, wapo ambao husaga juisi sokoni na kisha wanajiwekea maji na barafu na kuanza kutembeza mitaani na kuuza. Ndio kigezo cha hatari kinapoanza, pale ikiwa kanuni za kufikia usalama kiafya isipozingatiwa. 

Kwa mana hiyo, kunatakiwa suala la usafi lizingatiwe, ili kulinda afya za watumiaji wote na ndipo inabeba tafsiri pana ya usalama wa umma. 

Pia na wale wanaokata matunda bila ya kuyafunika na kuuza, nao sio kisiwa, kanuni hiyo inawahusu sana wazingatie usalama wa afya za wateja wao kwa ujumla.