KURIPOTIWA kwa matukio ya utekaji na mauaji ya mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini kunaleta maswali mengi yanayokosa majibu.
Hapa nchini matukio hayo yalizoeleka kusikika katika nchi nyingine na kuonekana kama sinema kwa sababu Tanzania ni nchi inayosifika duniani kuwa ni ya amani na utulivu ndio sababu wageni wengi wanamiminika kuja kuitembelea na kuangalia vivutio vya utalii.
Utekaji na matukio ulioanza kujitokeza kwa sasa unaleta hali ya wasiwasi na kusababisha wananchi kuishi kwa wasiwasi kwa sababu hawajui lini yatawakuta.
Hali hii inasababisha hata baada ya watu kuhofia kufanya shughuli za maendeleo kwa kuwa hawafahamu wakati gani wanaweza kupatwa na mkasa.
Kuibuka kwa matukio haya kumesababisha watu kunyoosheana vidole bila kujua kiini cha tatizo hilo ni nini.
Takribani miaka mitatu iliyopita kuliibuka matukio ya watu kutoweka wakiwamo waandishi wa habari na wengine mpaka leo hawajulikani walipo.
Hali ilirudi kuwa shwari, lakini sasa imeanza kuibuka tena na kwenye jamii yamepamba moto kutokana na taarifa zinazoripotiwa kila mara matukio hayo kufanyika.
Kinachosikitisha zaidi hata watoto wasiokuwa na hatia wameingizwa kwenye matukio hayo na kupotezewa maisha yao.
Matukio ya hivi karibuni yameonesha majaribio ya watu kutekwa, wengine kuuawa kwa kudhania kuwa ni watekaji na tukio lingine ni la mfamasia aliyeuawa na kisha mwili wake kukutwa ukiwa umefukiwa karibu na nyumba yake.
Vitendo hivi vinasikitisha na sasa imeonekana ni kama wimbi linalovuma la utekaji na mauaji.
Kwa hivi karibuni Mkoa wa Dodoma, kumeripotiwa matukio kadhaa ya kinyama na mauaji na watu kuhoji kuna upepo gani mbaya umeikumba nchi yetu.
Wanaotekeleza unyama huo haifahamiki kama wanafanya kwa kulipiza kisasi au kwa sababu za kishirikina.
Huku Jeshi la Polisi likifanya uchunguzi kuhusu matukio hayo, inasikitisha kuona vikiendelea kufanyika na wanaofanya vitendo hivyo bado ni watu wasiojulikana.
Watu kutekwa, kutoweka na kuondolewa uhai sasa zimekuwa taarifa zinazotawala vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii.
Matukio haya yalianza taratibu, lakini yanakoendelea yanaweza kuwa makubwa na kusababisha wananchi kuhofia kutembea kwa amani kwenye nchi yao.
Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi kuhusu matukio hayo na imani ya wananchi kuwa waliofanya vitendo hivyo vya kinyama watakamatwa ili sheria ichukue mkondo wake.
Damu za watu haziwezi kupotea bure, hata kama waliofanya vitendo hivyo watakuwa wamekimbia kwenda maeneo ya mbali, lazima watajulikana.
Wananchi pia ni lazima tutoe ushirikiano kulisaidia Jeshi la Polisi kuwapata wahalifu hao ili nchi yetu isiingie doa.
Sisi sote ni walinzi na tunapotoa ushirikiano kazi ya kupatikana kwa wahalifu hao itakuwa rahisi. Hakuna anayependa kuona uhai wa mtu ukiondolewa kwa sababu za chuki na ubinafsi au ushirikina.
Tanzania ni nchi ya kisiwa cha amani na amani hii iendelee kudumishwa ili tuendelee kupokea wageni wanaokuja kujifunza kwetu jinsi ya kuishi kwa umoja na upendo.
Viongozi wa dini ni watu wanaoaminika na waumini wao, wanapoongea ni sawa na kutoa ujumbe kutoka kwa Mungu. Hivyo ni jukumu lenu kuhakikisha watu wanarudi katika hofu ya Mungu na kuepuka vitendo vya kinyama.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED