Kuiba misalaba, mashada ya maua makaburini ni laana

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:59 AM Jun 06 2024
Misalaba iliyokamatwa ilioibwa kwenye makaburi.
Picha: Mtandao
Misalaba iliyokamatwa ilioibwa kwenye makaburi.

KWA miaka ya hivi karibuni kuna kukithiri kwa wizi wa mashada ya maua makaburini, na ung'oaji wa misalaba unaofanywa na baadhi ya vijana kwa lengo la kuuza vyuma chakavu.

Katika baadhi ya makaburi ambayo hayalindwi, kumekuwa na aina hiyo ya wizi hasa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha, lakini kwa sasa hali imeendelea kuwa mbaya, safari hii jiji la Dodoma limekumbwa na kadhia hiyo.

Katika kata ya Chang'ombe, jijini humo wamelalamika kuzuka na kukithiri kwa ung'oaji misalaba kwenye makaburi unaofanywa na baadhi ya vijana wa huko.
 Wakazi hao wakasema kuwa wezi hao, wamekuwa pia wakibomoa zege na kuchukua nondo, kisha kwenda kuziuza kama chuma chakavu.

Wakasema kutokana na hali hiyo, hivi sasa baadhi ya ndugu wanaofiwa kwenye kata hiyo, wanalazimika kuweka alama za mawe kwenye makaburi ya wapendwa wao waliofariki, au misalaba ya mbao ambayo wanadai imekuwa ikiliwa na mchwa

"Inatusikitisha sana kutokana na vitendo hivyo ambavyo ni sawa na udhalilishaji wa ndugu zetu waliokufa kwa kuibiwa alama zao, ambazo ni muhimu kwa kumbukumbu kujua walikozikwa," alisema mmoja wa wakazi, Hamis Ramadhani.

Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa Mazengo, iliyopo kata hiyo, Abdallah Mtosa, amekiri wakazi kufikisha malalamiko ofisini kwake kuomba kuwadhibiti aliowaita ‘vijana’.

Akasema kuwa, watafanya kazi hiyo kwa kushirikiana na jeshi la Polisi. Akasema vijana wengi maeneo hayo wamekuwa na tabia mbaya ya kucheza kamari, kubeti, kukaa vijiweni, badala ya kutumia muda wao kufanya kazi.

Ukweli ni kwamba, tabia hii haipo Dodoma tu, kama nilivyosema imeenea maeneo mengi nchini, hasa mijini na katika makaburi ya kijamii ambayo hayalindwi.

Biashara ya chuma chakavu kwa kiasi kikubwa ndiyo imesababisha kukithiri kwa biashara hii, ambapo mbali na kung'oa misalaba, vijana ambao kwangu mimi sitakuwa na jina lingine la kuwaita zaidi ya wezi, wamekuwa pia wakirandaranda mitaani na kuimba sufuria, sahani na bakuli zilizotengenezwa kwa bati.
 Pamoja na haya yote huwezi kulaumu kuwepo kwa biashara hiyo kuwa ndiyo kunasababisha hivyo.

Huwezi kukataza biashara ya visu kwa sababu eti kuna mtu amempiga mwenzake kisu, badala yake aliyefanya hivyo ndiye atabeba msalaba, kwani hakuwa na matumizi sahihi ya bidhaa hiyo.

Kwa hiyo kinachotakiwa hapa ni kudili na wezi hao, na si kupiga marufuku biashara ya chuma chakavu.

Nasema hivi kwa sababu baadhi ya watu wataona kama ni hivyo basi biashara hiyo ipigwe marufuku, la hasha. Cha kufanya ni Jeshi la Polisi, Polisi Jamii na Wananchi wote kwa ujumla wote nchi nzima wawe macho na wahalifu hawa.

Kinachosikitisha ni kwamba baada ya vijana wanaofanya uhalifu huo wanafahamika ni wa hapo hapo mitaani, lakini hawakamatwi si kama hawajulikani, lakini damu nzito kuliko maji, ni vijana wetu, na wengine wanaogopa lawama kwa majirani zao wakiwataja au kuwakamata.

Na si misalaba tu, imefika wakati wanasubiri watu waondoke makaburini, wanakwenda kuzoa mashada ya maua ambayo yamewekwa na kwenda kuyauza.

Nimezunguka kote, lakini narejea kuwakanya, kuwaambia na kuwatahadharisha vijana wenye tabia hiyo, kuwa pamoja na kwamba ni uhalifu kama mwingine wowote, hivyo ni kosa la jinai, lakini kwa utamaduni wa Kiafrika na dini  zote, kuiba kitu cha mtu aliyefariki, au kuiba kitu chochote makaburini ni dhambi kubwa isiyosameheka mbele za Mungu na ni laana.

Inawezekana hata huko mbele ya safari kwenye maisha kijana akaacha mambo hayo, akawa na familia, lakini asiwe na bahati yoyote, bali ni mikosi kila kukicha, kumbe inatokana na laana ya miaka mingi iliyopita ya kuiba makaburini.