Jamani kichocho siyo kurogwa

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 08:59 AM Jun 12 2024
Maji yaliotuama yanayosababisha kichocho.
Picha: Mtandao
Maji yaliotuama yanayosababisha kichocho.

MACHI mosi mwaka huu, kampeni ya kitaifa ya kuielimisha jamii kuhusu kichocho na minyoo ya tumbo, ilishika kasi.

Ikifanyika katika maeneo mbalimbali, inawalenga watoto wenye chini ya miaka 15 kupatiwa chanjo dhidi ya magonjwa hayo. 

Ikumbukwe ni kazi ya  kila mwaka, inayofanyika kwenye shule za msingi, vituo vya afya, zahanati na maeneo yanayotengwa na serikali. 

Kuna nyakati wataalamu wametembelea  nyumbani kuwahimiza wazazi na walezi kuwafikisha watoto vituoni kupatiwa chanjo dhidi ya magonjwa hayo.

 Chanjo hiyo ambayo inagharamiwa na serikali, inatolewa ili kuwaepusha na maradhi ili wawe na afya njema na akili timamu. 

Kwa hiyo wazazi na walezi waitikie wito ili watoto wao wapate chanjo dhidi ya magonjwa hayo kwani yanazuilika na hata kutokomezwa. 

Zipo taarifa kuwa kuna wananchi ambao wanasikiliza uvumi kuwa dawa hizo husababisha ugumba, yote hayo yana lengo la kukwamisha juhudi za serikali za kuwachanja watoto. 

Pamoja na kukwamisha mpango huo bado wataalamu wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kwenye vituo vya afya na vyombo vya habari kuhusu chanjo na jinsi  ya kujikinga na magonjwa hayo hasa kwa watoto na kuhimizwa wawapeleke kwenye chanjo kila mwaka. 

Lengo lao ni kuondoa imani potofu miongoni mwao kuwa magonjwa hayo yanatokana na kurogwa.

Wapo watu wanaoamini kuwa mtoto akikojoa damu inakuwa ni dalili za kuwa amefikia umri wa kupevuka  na wengine  wanahusisha na imani za ushirikina kuwa wamelogwa.

Wanaanza  kumpeleka kwa mganga wa kienyeji, wakiamini kuwa kule ndiko kuna tiba sahihi. 

Jamii inapaswa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya ambao mara kwa mara wanawahimiza watoto  kupelekwa kituo cha afya kupata kinga kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kutokomeza magonjwa hayo. 

Watanzania waelewe kuwa kichocho ni ugonjwa ambao unaenezwa na konokono wanaoishi kwenye madimbwi na maji yanayotuama. 

Ikumbukwe dalili zake ni muwasho wa ngozi katika viungo, kupata homa, udhaifu na baadaye damu kwenye kinyesi, mkojo na kuumwa na tumbo. 

Aidha mgonjwa anaweza kuwa na mafua, kuumwa misuli, pia  ukurutu, kikohozi na maumivu ya tumbo. 

 Kichocho, kinatibiwa kwa dawa aina ya praziquantel, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO). 

Maambukizi ya minyoo na kichocho yanaweza kumpata mtu kupitia kwa binadamu iwapo kinyesi na haja ndogo zitakuwa na wadudu (minyoo) na mayai ya konokono yanayotagwa kwenye madimbwi, mifereji na mito na ya minyoo inayopatikana kwenye maeneo hayo. 

Kwa mujibu wa wataalamu jamii inaweza kujikinga na maradhi hayo kwa  kuhakikisha inatumia majisafi na salama na kuepuka mazingira machafu.

 Kichocho huwapata zaidi wavuvi, wakulima, watoto wanaocheza kwenye maji yasiyo salama na watu wanaotumia maji hayo.

  Kuna miradi wa kudhibiti wa kichocho ambayo imeanzishwa katika maeneo yenye maziwa na visiwa kwa lengo la kuhakikisha magonjwa hayo yanatokomezwa na jamii inakuwa salama na afya bora. 

Taarifa za Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yasiyopewa Kipaumbele, maradhi  hayo yanasababisha madhara kwa binadamu ikiwamo ulemavu wa muda mrefu.

Aidha, huathiri maendeleo na makuzi ya watoto, kupunguza uwezo wa utendaji kazi na pia inachangia magonjwa ya saratani hivyo kusababisha umasikini kwenye jamii kutokana na gharama kubwa za tiba. 

Athari nyingine ni kuharibika  mimba, unyanyapaa hasa kwa wasichana na wanawake wagumba, utapiamlo kwa watoto, upungufu wa damu mwilini, udhaifu wa aina mbalimbali.

Matatizo mengine, ni presha ya ini, saratani ya  kibofu cha mkojo, upofu na uwezo duni wa kuelewa masomo na kujifunza.

 Hivyo shime jamii, iache imani potofu za kuhusisha magonjwa hayo na ushirikina na kuwapuuza wanaovumisha chanjo zinasababisha ugumba na kuua nguvu za kike na za kiume.

Kufanya hivyo ni kukwamisha juhudi za serikali za kutaka kizazi cha sasa na kijacho kuwa na afya bora kwa kutokomeza magonjwa hayo.